Baada ya timu ya Geita Gold Sport kufanikiwa kuingia hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la FA, kocha mkuu wa timu hiyo, Selemani Matola, ameibuka na kusema anatamani kukutana na timu yake ya zamani, Simba.
Matola alikuwa kocha msaidizi wa Simba kabla ya kutangaza kuachana nayo mwishoni mwa mwaka jana kwa kile alichokieleza kutoelewana na aliyekuwa kocha mkuu, Muingereza, Dylan Kerr ambaye naye mapema mwaka huu alitimuliwa.
Tangu Matola akabidhiwe mikoba ya kuinoa timu hiyo ya mkoani Geita, ameweza kuiongoza vizuri katika michuano mbalimbali, ambapo katika Ligi Daraja la Kwanza amefanikiwa kumaliza ligi hiyo wakiwa kileleni mwa Kundi C.
“Simba ni timu yangu ninayoipenda na ndiyo maana nataka kucheza nayo, si kwamba nataka kulipiza kisasi bali nataka kuwaonyesha kwamba nina uwezo, ndiyo maana naomba sana kukutana nao katika robo fainali, lakini si hiyo tu, bali timu yoyote nikikutana nayo nimejipanga kutembeza kichapo,” alisema Matola.
0 COMMENTS:
Post a Comment