March 28, 2016


Siku chache baada ya wachezaji wa Coastal Union kugoma kwa kutolipwa mishahara yao ya miezi mitatu, mapya yameibuka baada ya kiungo Mcameroon, Youssouf Sabo kulia na timu hiyo kumnyima haki yake ya kimkataba.

Sabo ambaye aliwahi kufanya majaribio kwa wiki kadhaa na Yanga, ameeleza mazito kuhusu manyanyaso anayokumbana nayo ikiwemo kunyimwa pasipoti yake, kulipwa nusu ya mshahara tangu asajiliwe pamoja na hela ya usajili ambayo mpaka mkataba wake unafika ukingoni hajalipwa.

Katika mahojiano maalum, Sabo alisema ameshindwa kuchangamkia ofa mbili tofauti kutoka timu ya Motherwell ya Scotland na Arabe Contactor ya Misri ambayo alikwenda Elias Maguri wa Stand kutokana na uongozi wa Coastal kumbania paspoti.

Aidha, bado hajui ni lini timu hiyo itampa madai yake ya fedha za usajili na mshahara kwani ametumia kila njia lakini ‘unjanja- ujanja’ wa viongozi umekuwa mwingi.

“Mpaka sasa ninawadai dola 2,000 (Sh mil 4.3) za usajili, walinipa dola 1,000 na wakasema wangenimalizia muda mfupi lakini kila nikidai wananipiga danadana. Mpaka nimefika kwa mwenyekiti lakini wote wananichenga tu.

“Msharaha wangu ni dola 1,000 (Sh mil 2.1) lakini tangu nisajiliwe sijawahi kupewa mshahara mzima, ninapewa nusu yake, nikiuliza wanasema timu haina hela eti nitalipwa zote pindi wakichukua hela ya udhamini (wa ligi kuu- Vodacom na Azam TV), ligi inaisha na sidhani kama kweli hela ya udhamini mpaka sasa ipo tena.

Wakala wangu (Oscar Chale) amezungushwa hadi amechoka sasa,” alisema na kuongeza:

“Wameninyima na pasipoti yangu, kuna ofa mbili kutoka Scotland na Misri, zote nimeshindwa kwenda majaribio kwa kuwa sikuwa na pasipoti.” 

Coastal kupitia meneja wake, Muddy Kiliwasha, ilisema: “Ni kweli paspoti yake tunayo. Kisheria kumbukumbu za mwajiriwa zote zinatunzwa na mwajiri wake, Sabo bado mkataba wake haujaisha na atapewa utakapoisha kama wachezaji wengine, siyo yeye tu, kila mmoja atapewa yake.

“Ishu ya hela siyo kweli, kama unakumbuka karibu wachezaji wote waligoma tukawalipa na hakuna anayetudai.”

Source: Championi

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV