Ishu ya mtafaruku baina ya Kocha wa Simba, Jackson Mayanja na beki wa timu hiyo, Abdi Banda bado haijatolewa maamuzi baada ya kila mmoja kwa upande wake kutoa maelezo.
Katika hilo beki huyo ambaye aliwasilisha barua yake ya maelezo Machi 24, mwaka huu kwa kile kilichotokea kwenye mechi dhidi ya Coastal Union, amesema kwamba kwa sasa anasikilizia tamko litakalotolewa na uongozi wa timu hiyo na kama itakuwa adhabu kali atajua nini cha kufanya.
Ilielezwa kwamba, Banda na Mayanja walivurugana kwenye mechi ya Coastal, Tanga ikidaiwa kuwa beki huyo aligoma kupasha mwili kwa ajili ya kuingia uwanjani.
“Barua yangu ya maelezo tayari nimeshawapa, sasa hivi nasikilizia kitakachotokea, siwezi kuongea mengi maana kila kitu changu nimekieleza kwenye hiyo barua, kama kutakuwa na adhabu labda kama ya Isihaka (Hassan), ndiyo nitajua nini cha kufanya, nafikiri muda huu tuupe nafasi uongozi,” alisema Banda.
Kabla ya Banda, mwezi mmoja uliopita beki mwingine wa Wekundu hao, Isihaka alipewa adhabu ya kusimamishwa kazi na kuvuliwa unahodha usaidizi kutokana na tatizo kama hilo la utovu wa nidhamu ingawa sasa amerejea kwenye kikosi hicho mwishoni mwa wiki iliyopita.
0 COMMENTS:
Post a Comment