March 26, 2016

MAGURI
Mshambuliaji Elias Maguri amebakiza miezi miwili tu katika mkataba wake na Stand United, amesema hana mpango wa kubaki kutokana na jinsi mambo yanavyokwenda.

Hadi sasa Maguri ana mabao 10 katika Ligi Kuu Bara huku akiifungia Taifa Stars bao moja lakini amekuwa hapati nafasi katika kikosi cha kwanza cha Stand United kwa sababu za utovu wa nidhamu kwa mujibu wa kocha wake, Patrick Liewig.

Maguri amesema itakuwa ndoto kwake kubaki Stand na sasa anatazama kujiunga na timu nyingine kabisa kwa kuwa hana kawaida kucheza zaidi ya msimu mmoja katika timu moja ligi kuu.

Hata hivyo, sababu nyingine ambayo Maguri hakuitaja ni mfarakano wake na Liewig ambaye amekuwa akimweka benchi mara kwa mara kikosini. 

“Sioni sababu ya kuficha ukweli, mkataba wangu una miezi miwili tu pale Stand na sijaongea na yeyote klabuni hapo kuhusu ishu ya mkataba. Siko tayari kubaki pale.

“Chaguo langu la kwanza kwa sasa ni kuangalia nje zaidi, Tanzania ni chaguo la pili, endapo mambo hayatakwenda vizuri basi nitaangalia timu nyingine hapa nchini lakini siyo Stand,” alisema Maguri.

“Kwanza ukiangalia takwimu sina kawaida ya kukaa kwenye timu zaidi ya msimu mmoja, kote nilikopita nimecheza msimu mmoja, labda Polisi Mara (timu iliyomuibua) nilikaa miaka miwili.”

Maguri alitokea Simba kwenda Stand msimu uliopita, kabla ya hapo alizichezea Ruvu Shooting na Tanzania Prisons kwa nyakati tofauti.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV