March 26, 2016


Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, amesema ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya Chad katika mechi ya kufuzu Kombe la Afrika 2017, haukuja kirahisi na sasa watapambana kuhakikisha wanashinda mechi ya Jumatatu. 

Mechi hiyo ilichezwa Jumatano iliyopita kwenye Uwanja wa Idriss Mahamat Ouya jijini N’Djamena, Chad ambapo Samatta alifunga bao hilo pekee dakika ya 30 katika mchezo huo wa Kundi G.

Akizungumza mara baada ya Taifa Stars kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakitokea Chad, Samatta alisema wapinzani wao walikuwa vizuri lakini walitumia vizuri kosa la Chad na kupata bao. 

“Licha ya kuwafunga kwao, hatutakiwi kubweteka na ushindi huo wa bao moja, tunachotakiwa ni kukaza buti katika mechi ya marudiano tutakayocheza hapa kwetu hiyo Jumatatu.

“Sisi hatutawadharau, tutawakazia kwa kucheza kufa na kupona, maana hiyo ni kama vita, ni lazima tupambane mbele ya macho ya Watanzania,” alisema Samatta.

Taifa Stars sasa imefikisha pointi nne katika Kundi G huku Misri ikiwa na pointi sita na Nigeria ilikuwa na nne kabla ya mechi yao ya jana. Chad haina pointi. Taifa Stars na Chad zinacheza keshokutwa Jumatatu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV