Pamoja na mshambuliaji wa Simba, Mganda, Hamisi Kiiza kupitwa bao moja na mshambuliaji wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe kabla ya mechi ya jana, lakini kitwakimu inaonekana Mganda huyo yupo juu ya Tambwe kwa ufungaji.
Kwa sasa Tambwe ambaye ndani ya msimu huu amepiga ‘hat trick’ mbili, ndiye kinara wa mabao akiwa nayo 17 akifuatiwa na Kiiza mwenye mabao 16 akiwa na hat trick moja.
Kinachomfanya Kiiza amfunike Tambwe licha ya kuzidiwa idadi ya mabao ni kufunga mabao mengi kwenye viwanja vya nje ya Dar es Salaam ambapo wachezaji wengi na makocha wamekuwa wakilalamika kuwa ni vibovu na kutotoa fursa ya kucheza soka zuri.
Katika mabao yote 16, Kiiza amefunga manne kwenye viwanja vya mikoani tena ambayo yameipa pointi tatu Simba, mechi hizo ni dhidi ya African Sports kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Simba ikishinda bao 1-0, alifunga bao la pili uwanjani hapo Simba ilipocheza dhidi ya Mgambo na kushinda mabao 2-0.
Akafunga mabao mawili dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga ambapo Simba ilishinda mabao 2-1.
Upande wa Tambwe, katika mabao yake 17, amepiga bao moja tu nje ya Uwanja wa Taifa, tena Yanga haikushinda katika mchezo huo dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya ambapo matokeo yalikuwa ni sare ya mabao 2-2.
0 COMMENTS:
Post a Comment