Na Saleh Ally
MECHI nane za Ligi Kuu England zinapigwa leo kwenye viwanja na miji mbalimbali ya nchini England lakini gumzo linaendelea kubaki katika mechi ya watani ya North London Derby.
London Derby ni mechi inayowakutanisha Arsenal dhidi ya Tottenham Hotspurs, mechi ambayo safari hii inachezwa leo, Spurs wakiwa nyumbani White Hart Lane.
Jiji la London lina zaidi ya mechi tano za derby, zile za West London Derby inayoweza kuzikutanisha kati ya Chelsea na QPR au Chelsea na Fulham. Pia kuna South London Derby wanapokutana Crystal Palace dhidi ya Charlton Athletic.
Lakini bado derby ya Kaskazini imeendelea kuwa kubwa na maarufu zaidi na safari hii utamu unaongezeka kwa kuwa Spurs inaonekana kuwa katika kiwango bora zaidi ya Arsenal.
Raha zaidi ya hiyo, timu zote mbili zimecheza mechi zao za mwisho na kupoteza michezo yao. Hivyo kila moja imetawaliwa na uchungu wa kufungwa huku ikiwa na hamu ya kutwaa ubingwa.
Arsenal inaingia kwenye mechi ngumu ya derby baada ya kuwa imepoteza mechi mbili mfululizo. Kwanza ilifungwa kwa mabao 3-2 ikiwa ugenini dhidi ya Manchester United, mwisho ikapoteza tena kwa kuchapwa 2-1 na Swansea nyumbani.
Spurs wana rekodi nzuri zaidi, ingawa nao walitandikwa bao 1-0 wakiwa ugenini dhidi ya West Ham United katika mechi ambayo ilionyesha kuwashangaza.
Utamu wa mechi hiyo, kwa rekodi, Spurs inapewa nafasi kubwa ya kushinda kwa kuwa kama utaangalia mechi zake nane zilizopita, imeshinda sita na kupoteza mbili dhidi ya West Ham na Leicester City.
Katika msimamo wa Ligi Kuu England, Spurs ina matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa ikiwa katika nafasi ya pili na pointi 54, Leicester wanaongoza wakiwa na pointi 57.
Matumaini hayajafika mwisho kwa Arsenal hata kama kocha wao, Arsene Wenger, anaonekana kukata tamaa baada ya kupoteza pointi sita katika mechi mbili mfululizo.
Rekodi ya mechi nane zilizopita pia imekuwa ya mabonde mengi. Kwani imeshinda mechi mbili, sare tatu na kupoteza mechi tatu. Swali linakuja hapo, kwamba kweli itauweza mziki wa Spurs chini ya Kocha Mauricio Pochettino?
Kikubwa ambacho kila mpenda soka anaweza kujifunza ni kwamba mpira wa England kila mechi sasa ni ngumu na hakuna kinachoamuliwa tena kwa rekodi za nyuma. Timu nyingi zilifanya vema hata kushinda mechi sita au saba, lakini zikafungwa na timu ambayo haikuwa imeshinda hata mechi moja.
Kwa kifupi mechi ya leo, itakuwa haina mwenyewe na unajua inapokuwa mechi ya watani au yenye upinzani mkubwa, ni suala la anayekosea, basi mwenzake anamuadhibu.
Lakini kwa hesabu za umakini, unaweza kuwapa nafasi Arsenal ambao wachezaji hawatakuwa tayari kuwa na “hat trick” ya vipigo. Ingawa ugumu utaongezeka kwa kuwa Spurs pia hawatataka kupoteza mchezo wa pili.
Mechi ni ngumu, lakini Spurs inaendelea kulindwa na rekodi nzuri ya timu iliyoshinda zaidi ndani ya mechi nane zilizopita, wakati Arsenal ndiyo timu kati ya nne za juu kileleni iliyofanya vibaya zaidi katika mechi zake tano zilizopita.
Kama mbinu za makocha zitafeli, bado kila upande una wachezaji wenye uwezo binafsi. Angalia Harry Kane, Dele Alli, Nacer Chadli na wengine kwa upande wa Spurs au Arsenal na watu kama Mesut Ozil, Olivier Giroud, Joel Campbell, Theo Walcott na wengine, wakiamka vizuri, inaweza kuwa si kazi ndogo.
MECHI NANE ZA MWISHO
TOTTENHAM:
West Ham 1-0 Spurs
Spurs 2-1 Swansea
Man City 1-2 Spurs
Spurs 1-0 Watford
Norwich 0-3 Spurs
C Palace 1-3 Spurs
Spurs 4-1 Sunderland
Spurs 0-1 Leicester
ARSENAL:
Arsenal 1-2 Swansea City
Man Utd 3-2 Arsenal
Arsenal 2-1 Leicester
Bournemouth 0-2 Arsenal
Arsenal 0-0 Southampton
Arsenal 0-1 Chelsea
Stoke 0-0 Arsenal
Liverpool 3-3 Arsenal
IMEKUSANYA POINTI
Spurs: Katika mechi zake nane, Spurs imeshinda sita na kupoteza mbili, hivyo kukusanya pointi 18.
Arsenal: Hakika kikosi cha Arsenal hakina mwendo mzuri, katika mechi nane kimeshinda mechi mbili, sare tatu na kupoteza mechi tatu, hivyo kukusanya pointi tisa tu!
MECHI 10 ZA MWISHO ARSENAL VS SPURS TOKEA 2011:
8 Nov 15 Arsenal - Tottenham 1-1
7 Feb 15 Tottenham - Arsenal 2-1
27 Sep 14 Arsenal - Tottenham 1-1
16 Mac 14 Tottenham - Arsenal 0-1
1 Sep 13 Arsenal - Tottenham 1-0
3 Mac 13 Tottenham - Arsenal 2-1
17 Nov 12 Arsenal - Tottenham 5-2
26 Feb 12 Arsenal - Tottenham 5-2
2 Okt 11 Tottenham - Arsenal 2-1
20 Apr 11 Tottenham - Arsenal 3-3
MSIMAMO WA NYUMBANI:
P Pointi
1 Leicester 14 29
2 Man City 14 28
3 Tottenham 14 28
4 Man United 14 28
5 Arsenal 14 27
6 West Ham 14 26
7 Southampton 14 23
8 Stoke City 14 23
9 Chelsea 14 20
10 Liverpool 13 20
MSIMAMO WA UGENINI:
P Pointi
1 Leicester 14 28
2 Tottenham 14 26
3 Arsenal 14 24
4 Everton 13 22
5 Liverpool 14 21
6 West Ham 14 20
7 Man Utd 14 19
8 Chelsea 14 19
9 Man City 13 19
10 Crystal Pal 14 19
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment