March 4, 2016


Na Saleh Ally
WANASAYANSI wanavitaja baadhi ya vyakula vinavyosaidia kuinua uharaka wa kazi ya ubongo wa mwanadamu, kama utavisikia unaweza kushangazwa lakini hiyo ndiyo inakuwa hali halisi.

Baadhi ya vyakula vinavyosaidia ubongo wa mwanadamu kuongeza kasi ya utendaji wake ni pamoja na samaki wadogo wenye mafuta, nyanya, zabibu yote hii ni katika kutafuta vitamin C, E na nyinginezo.



Kwa kuwa mimi si daktari, wala si taaluma yangu kawaida napenda kujifunza kila nitakachoweza ili angalau kujua jambo fulani. Kabla sijasoma suala hilo, hakika sikuwa nikiona umuhimu wowote wa kula mbegu za maboga au aina yoyote na “nuts” kama korosho, karanga na nyinginezo. Pia sikuwa nikiona umuhimu wa kula nyanya hasa zilizochemshwa.


Sasa ninafanya hivyo kwa kuwa nimejifunza baada ya kujielimisha na baada ya hapo nikauliza zaidi. Maisha ni kujifunza kuliko kuishi kama unajua sana, ndiyo maana nimekuwa nikishangazwa sana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuona mambo yake mengi yanaweza kwenda kwa siri badala ya kujifunza uwazi unaoweza kusaidia.

Kila mara nimesisitiza TFF ni ya Watanzania ni ya umma na si mali ya mtu mmoja. Hivyo vizuri pia ikawatumikia Watanzania badala ya mtu mmoja au kikundi cha watu fulani.

Kama unakumbuka, mapato ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara zilikuwa zikitangazwa kila baada ya mechi hizo, lakini siku hizi kumeibuka utamaduni mpya wa kuficha kilichopatikana.

Kama itatangazwa ni kwa baadhi ya mechi fulani hivi na baada ya hapo hakuna ambacho kinaweza kufanyika. Juhudi za Championi kuhakikisha inaendelea kupata taarifa za mapato hayo zimegonga mwamba huku ikionekana TFF haitaki kuyatoa.

Sasa najiuliza, TFF inataka kuficha nini na kwa faida ya nani? Lengo hasa au faida ya kuficha kinachopatikana itakuwa inamsaidia nani? TFF yenyewe au klabu husika?

Kipindi hiki cha serikali ya awamu ya tano ambayo inasisitiza ulipaji wa kodi bila ya kukwepa, ndiyo kipindi ambacho TFF wanaona ni sahihi kuficha mambo ambayo walikuwa wakiyatoa hadharani!

Najiuliza au TFF sasa wanaanza kukubaliana na Yanga kwamba kuingia mkataba wa TV, kumesababisha timu kukosa mapato? Kama ni hivyo nini njia mbadala na kwa nini wanaendelea kuficha?

Najiuliza tena, TFF imeamua kuficha mapato kwa kuwa wanaona aibu kuna mechi za ligi zinaingiza hadi Sh laki moja tu? Je, wakificha ndiyo itasaidia kuleta mabadiliko?

Bado pia najiuliza, kwamba tumesikia kuna watu kutoka kwenye vyama na mashirikisho wamekuwa wakihusika na uuzwaji wa tiketi za wizi. Je, hiyo inasaidia kuwaficha au kuwarahisishia kazi zao kufanyika vizuri?

Huenda ikawa ni shida sana kupata jibu sahihi badala yake nikaishia kujiuliza maswali hayo bila kuchoka. Ushauri wangu ili TFF kusaidia kuepukana na maswali ninayojiuliza, basi warejeshe utaratibu ulioanzishwa tokea kipindi cha Leodeger Tenga alipokuwa Rais wa TFF, akaweka uwazi.

TFF haina haja ya kufanya siri huenda kwa kuhofia changamoto. Maana nakumbuka baada ya kuanza kutangazwa kwa mapato na makato katika mechi hasa kubwa za Yanga na Simba, ndipo tulianza kugundua kuna watu walikuwa wakichota fedha bure tu.

Uchambuzi ulisaidia kuondolewa kwa gharama nyingi zisizokuwa na msingi na “wapigaji” wakabanwa na mwisho klabu zikaanza kufaidika na jasho lao angalau kwa asilimia 50.

Sasa hivi mambo si hadharani tena, kwa nini iwe leo. Vizuri kabisa TFF irudi katika uwazi ilioukuta kutoka kwa Tenga na Watanzania wataarifiwe kuhusiana na mapato hayo.

Uwazi unaweza kusaidia mabadiliko kutokana na mawazo hasa baada ya watu kuona na kujifunza jambo. Kufichaficha ndiyo mwanzo wa uovu au kutengeneza mianya ya ukwepaji kodi na uchotwaji wa mapato.

1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic