Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wachezaji wa Stand United, juzi walitwangana makonde wakati wa mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Iyunga.
Katika mazoezi hayo ya kujiandaa na mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Prisons, beki Assouman David, alimchezea faulo Frank Khamis ambaye uvumilivu ulimshinda na kuamua kurusha ngumi zilizompata usoni David.
Kutokana na kurushiwa ngumi, David naye akaanza kujibu mashambulizi lakini wachezaji wenzao waliwawahi na kuwaamua kisha kuwapeleka kwa kocha wao mkuu, Mfaransa, Patrick Liewig ambaye alionekana kuchukizwa na kitendo hicho japokuwa aliwaruhusu waendelee kufanya mazoezi mpaka mwisho.
Alipofuatwa na gazeti hili, Liewig hakuwa tayari kuzungumza.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Benchi la Ufundi la Stand United, Muhibu Kanu, alisema: “Masuala kama hayo siyo mageni kutokea katika mazoezi, tunachofanya ni kukemea yasijirudie ili kila mmoja azuie hisia zake.”
0 COMMENTS:
Post a Comment