April 1, 2016Na Saleh Ally
KIUNGO wa Yanga, Simon Happygod Msuva sasa ana umri wa miaka 23, unaweza ukasema ni mmoja wa wachezaji vijana wa Tanzania ambao mwendo wao ni mzuri.

Msuva ni mfungaji bora wa msimu uliopita baada ya kufunga mabao 17 na msimu huu tayari amefunga mabao sita.
Kamwe hauwezi kusema Msuva ni mchezaji wa kubahatisha, hakika ni mtu anayejitambua na anafanya kazi yake kwa ufanisi.

Nimezungumzia kufunga tu, lakini unajua Msuva amecheza mechi nyingi Yanga, amekuwa akitoa pasi za ufungaji mabao na wakati mwingine Kocha Hans van Der Pluijm amekuwa akimtumia kama mtu wa kuwachosha walinzi au wa kumalizia kazi.

Utaona katika mechi nyingi ngumu anamuweka benchi, ili akiingia anakwenda kumaliza mchezo. Iwe kwa kuwapa presha wapinzani warudi nyuma au kusaidia kupambana na kupata zaidi.

MSUVA
Si rahisi kumuona Msuva hayuko fiti, mara kadhaa mashabiki wa Yanga wamekuwa wakimlalamikia kwamba amekosa au kukosea. Lakini utagundua, hajawahi kukata tamaa, mara zote anapambana tu hadi kieleweke.

Ukiangalia kwa undani, Msuva si mchezaji mkongwe. Miaka 23, iwe ya kweli au ya ‘passport’ lakini uhalisia unaonyesha ni mchezaji anayepaswa kutoka nje ya Tanzania katika kipindi hiki ambacho binafsi nakiita ndiyo mwafaka.

Kuna rafiki yangu mmoja alikuwa akiniuliza vipi Mrisho Ngassa hatambi tena akiwa Afrika Kusini. Huenda alifikiri kiwango cha soka nchini humo kipo juu sana, ndiyo maana Ngassa ameshindwa kuchomoza. Lakini akashangazwa na Bidvest kutunguliwa na Azam mabao lundo!


Ngassa ameenda baada ya kuwa amemaliza kila kitu. Lakini kama angeondoka nchini akiwa na miaka 23, hakuna ambaye angemzuia Ngassa kufanya anachotaka uwanjani katika mechi za Afrika Kusini.

Ngassa alichelewa kuondoka kwa kuwa alivikwa ‘ufalme’ akiwa Yanga na baadaye Simba. Wakati huo uliona alipata nafasi nyingi za kucheza nje ambazo hakuzipa kipaumbele au kuzitumia. Alifanya hivyo kwa kuwa mazingira ya Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla yalimfanya afikiri yeye ndiye yeye. Mashabiki wanalevya, hilo lazima tulikubali. 


Wanamsahaulisha mchezaji na kuanza kuhisi yeye ni mtu wa anga nyingine kabisa na ataendelea kuwa hivyo milele, jambo ambalo si kweli.

Ushindani sahihi wa kucheza soka nje ya Tanzania hasa katika nchi zilizopiga hatua kubwa kisoka ni mchezaji kuwa fiti, kuwa katika kipindi chake bora cha ushindani na umri ni moja ya vigezo vya msingi kabisa.

Mchezaji kutaka maendeleo ya soka au ndoto ya kucheza Ulaya wakati akiwa na miaka 30 ni kujidanganya au ni kupoteza muda bila ya sababu ya msingi.


Pia asitokee mtu akasema eti Msuva hakuna timu zinazomtaka, ndiyo maana anaendelea kubaki Yanga na kubaki Tanzania. Huenda anasubiri tena kusajiliwa na timu nyingine ya Tanzania pale atakapofikia miaka 30 na mashabiki wa Yanga watakapozidisha  kumzomea kwa kuwa wataanza kuona uwezo wake unaporomoka.

Soka ni biashara, Msuva anafanya vizuri uwanjani. Bado anatakiwa kuwa na watu maalum ambao watakuwa wanamuuza nje  ya Tanzania kwenye klabu mbalimbali ndani ya Bara la Afrika na nje. Hawa wawe watu wataalamu ambao watamtengenezea wasifu wake bora ikiwa ni pamoja na picha nzuri za video na zile za mnato.

Baada ya hapo wafanye kazi ya kumtafutia soko katika nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya, Asia na ikiwezekana Amerika Kusini. Ninaamini kuna baadhi ya timu zitatoa nafasi kwenda kufanya majaribio.


Kutofuzu  majaribio ni sehemu ya mabadiliko ya maendeleo. Anayeshindwa kufuzu huwa amejifunza jambo. Pia uwezo wake wa kufanya jambo hilo huongezeka.

Hakika, Msuva hapaswi kuendelea kusubiri ndoto zake zitimie ‘uzeeni’, mwisho atakwenda kuwa kichekesho. Mwisho wa ukweli wa mambo ni sasa.0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV