April 22, 2016


ALI KIBA (KUSHOTO) & DIAMOND (KULIA) WAKIWA NA MDAU WA MUZIKI MIAKA KADHAA ILIYOPITA KABLA DIAMOND HAJAWA STAA.

   
DIAMOND Platinumz ni mwanamuziki mkubwa Afrika, inatajwa kuwa msanii huyo ana timu nzuri nyuma yake ambayo imemwezesha kupata mafanikio mengi makubwa.

DIAMOND & ALI KIBA WALIVYO SASA

Ukiachana na Said Fella na Babu Tale, kuna mtu anaitwa Sallamambaye inaaminika ni mmoja wa watu muhimu katika menejimenti ya Diamond. Sifa yake kubwa inayotajwa kuwa ni mzuri kutengeneza ‘connection’ nyingi zilizompaisha Diamond kimataifa.

Mashabiki na wadau wengi hawamfahamu kiundani, siku za hivi karibuni staa mwingine wa Bongo Fleva, AY alimtaja Sallamkuwa meneja wake. Sallam amezungumza na gazeti hili na kufunguka mengi:

Championi: Unajulikana kwa jina la Sallam, umetokea wapi na ulianzaje umeneja?
Sallam: Naitwa Sallam Sharaf, nilizaliwa Dar na nikasomea Morogoro. Muziki nilianza muda mrefu tangu nikiwa Shule ya Forest, Morogoro. Tulikuwa na kundi letu la Watukutu, tulikuwa tuna-rap, liliundwa na Puzzo, Swedi na mimi nikijiita OG.


Watukutu ilikuwa ikileta ushindani wa wasanii wa Dar na Moro, wale wa Dar walikuwa ni kina Mr II, Hard Blastaz na Dilpomatz. Profesa Jay yeye alitambulika akitokea Moro akiwa katika Kundi la Simple Guyz. Baadaye likazaliwa kundi lingine la Ze don P la kina Squeezer, kulikuwa na ushindani mkali sana wa makundi kwa wakati huo.


Uliingiaje kwenye umeneja?
Mwanzo nilikuwa napenda kuandaa shoo, niliwahi kuwaleta Prezzo, Hudah Monroe (wa Kenya), Jay Martins (Nigeria), hapohapo kina AY na MwanaFA wakamchukua J wakafanya naye wimbo wa Bila Kukunja Goti halafu nikamuunganisha na Ommy Dimpoz wakafanya ile ngoma ya Tupogo. Hata video ya Bila Kukunja Goti niliisimamia mimi kishkaji tu.

Ulikutana vipi na Diamond?
Kwa kuwa nilikuwa tayari nina ‘connections’ zangu, mwaka 2013 nilipata tenda ya Clouds FM kuwaleta kina Iyanya, Jay Martins na Davido kwenye Fiesta nikiwa wakala, nikapewa hela yangu tukamalizana.

Baadaye Diamond akanipigia simu akasema anataka kufanya kazi na Davido, nikampa masharti yangu akayakubali, nikazungumza na menejimenti ya Davido, tukaelewana, kesho yake ikaenda kufanywa remix ya Number One.

Tukataka kufanya video ya hiyo remix lakini Ogopa Deejayz wakachelewa, Davido akarudi kwao na baadaye ikaenda kufanyika Nigeria. Baada ya hizo harakati, Tale, Fella na Diamond wakasema kama vipi tuungane, tutengeneze timu iendelee kuwa kubwa na tangu hapo ndiyo nikaanza kufanya kazi na Diamond.

Wasanii gani wengine unafanya nao kazi?
AY, MwanaFA ambao wameingia hivi karibuni lakini nilianza kufanya nao kazi tangu awali kabla ya Diamond. Wengine ni Harmonize, Raymond na wasanii wa WCB.

AY si mwepesi wa kukubali kusimamiwa, uliwezaje kukubaliana naye?
Najitahidi kufanya kazi yangu katika ubora siyo ilimradi ikamilike. AY ni mtu ambaye nipo naye sana kila sehemu kuliko hata Diamond, aliliona hilo na kwa kuwa anajua ushindani umekua ndipo akaamua awe na msimamizi wa kazi zake, maana yeye peke yake hawezi kusimamia kila kitu.

Mkataba wako na AY ukoje?
Sina mkataba na msanii yeyote, mikataba yangu ni ya kiimani, tufanye kazi tutalipana hivi na hivi na kama ukiamua kunidhulumu sawa tu. Ila sijawahi kudhulumiwa!

Kazi zako ni zipi kwa msanii na unafaidika vipi?
Meneja ni mfanyakazi wa msanii, unapokuwa msanii tayari wewe ni kampuni inayohitaji watu kama mameneja. Malipo ni katika asilimia ya kazi mnazozifanya, kila sanaa inayofanyika kupitia yeye lazima meneja awe na fungu lake.

Mfano AY au Diamond ni ‘brand’ kubwa, wana nguvu kubwa, unajua kuna asilimia yangu kama kawaida lakini kwa msanii mchanga anayetaka nimsimamie analazimika anilipe yeye.

Hivi kwa nini Diamond ana mameneja wengi?
Kwa Diamond hata mameneja watatu hawatoshi. Mfano juzi tulikwenda kwenye ziara Ulaya, hapo lazima uwe na meneja atakayedili na chakula, ratiba, ukumbi na mengine mengi.

Sisi tunakuwa tunapokezana, Tale pia ni meneja wa Tip Top na Madee, wakati huo mimi nakuwa na Diamond. Kuna muda Fella anakuwa na Ya Moto Band, tunakuwa tunabadilishana kama hivyo.

Unatumia njia gani kurahisisha kazi yako?
Ni kujiamini tu, huwa siogopi mtu, nikipewa nafasi naitumia vizuri, nazijua vizuri ‘CV’ za wasanii wangu.

Ikitokea Ali Kiba anahitaji ufanye naye kazi, utakubali?
Sina tatizo kabisa, akitaka tufanye kazi nitamweleza mahitaji yangu akikubali tutafanya kazi. Nilishawahi kukutana na Kiba, Nairobi, alinifuata akaomba tupige picha, sikuwa na kinyongo, tukapiga ikawa safi japokuwa ile picha aliitumia kunitukanisha baadaye.

Kivipi?
Hakuiweka yeye katika mtandao, aliitoa kwa mashabiki wake ambao wakasema nimeenda Nairobi kumfuata Ne-Yo halafu nikafukuzwa, wakasema mimi ndiyo niliomba kupiga picha na Kiba, ikawa gumzo sehemu nyingi. Ukweli nilikuwa na Ne-Yo na Diamond ambaye alikwenda pale kurekodi, yeye Kiba alikuwa Coke Studio.

Baada ya hapo ulishakutana tena na Kiba?
Ndiyo, akaniomba msamaha akasema yeye aliwatumia waiposti na hayo maneno waliweka wao.

Unamuonaje Kiba kimuziki?
Siwezi kusema anakosea wapi, maana kila msanii ana njia zake. Wimbo wake wa Mwana ni mkali na ulifanya vizuri yawezekana anakosea kwenye ‘market’. Kuna vitu lazima ulazimishe, hata Diamond yupo juu lakini hawezi kutoa kitu halafu akatulia tu akaacha watu wapende wenyewe.

Kila mtu ana staili yake yawezekana yeye hataki kwenda kwenye staili kama hiyo, ndiyo maana kuna muda huwa nasema huwezi kumfananisha Diamond na Ali kwa sababu wanaimba muziki wa tofauti.

Wote ni Bongo Fleva lakini staili zao ni tofauti, kwa mtu anayefuatilia muziki anaweza kugundua hilo.


 Ishu ya bifu la Diamond na Kiba ikoje?
Hakuna bifu kabisa, mimi nafahamu hilo. Wameshakutana na kusalimiana na hakuna chochote. Nasema kabisa wanapiga stori na wanaongea ‘fresh’ kabisa.




SALLAM


Mbona kama kuna picha ya kukwepana?
Kinachotokea ni kwamba watu wanawauliza kama wana bifu kwa hiyo wenyewe wanasema hawana bifu basi, lakini kwa kuwa hakuna maelezo mengi watu wanachukulia hivyo.
 

 
Ilidaiwa uongozi wa Diamond unafanya fitna ya kuzuia video za Kiba zisipigwe katika vituo vikubwa vya nje kama MTV na Trace, ni kweli?
Siyo kweli. Kiba na ana nguvu kubwa MTV na Trace kuliko Diamond kwa ajili ya Seven (ni mmoja wa wasimamizi wa Ali Kiba).

Seven alikuwa mfanyakazi wa MTV, anawajua watu wote wa MTV, hata yule bosi wa Trace wa sasa alikuwa chini ya Seven, ndiyo maana hata video yake ya Chekecha Cheketua ilichezwa wiki nzima mfululizo ikiwa ni ‘Exclusive’.

Wenzetu katika vituo wanaangalia vigezo vyao. Nikupe siri kuwa wakati naanza kazi na Diamond, alikuwa anabaniwa kweli zisipigwe kabisa hata Channel O.

Nani alikuwa anambania Dimond?
Siwezi kutaja jina lakini nyimbo zilikuwa zinapelekwa DStv hapo lakini anaambiwa hazina viwango, zinarudi. Aliyekuwa anafanya hivi ni Mtanzania na ni mhusika mkubwa wa muziki wa Tanzania.

Nini kilitokea baada ya kugundua hilo?
Nilimfuata nikamchana ‘live’ baadaye tukaamua kazi zetu kuzipitishia Nigeria kisha tukarudi hapa na kila kitu kikawa rahisi. Niwashauri watu kuwa wafanye kazi na watangaze kazi zao dunia ya sasa hakuna kitu kinachoenda chenyewe tu.

Skendo za Diamond huwa zinaathari kwenu?
Hatuathiriki, tunajua watu wanatafuta ‘booster’ kisha wanashindwa kuitumia.

Kwa nini Bongo Fleva imechelewa kutoka kimataifa?
Watu wanapenda vya bure, ‘nisaidie’ zilikuwa nyingi, wenzetu wanatoa fedha ili waingize fedha.

Suala la kwenda nje kutengeneza video limekuwa likizungumzwa sana, unalizungumziaje hilo?
Hapa kwetu vibali ni tatizo, mfano gari za polisi, kupata benki au kituo cha polisi, bado jamii yenyewe haijaona kama muziki ni biashara kubwa. Wenzetu kule mtu anakuachia nyumba ya thamani ya mamilioni, lakini hapa huwezi kuikuta na kama ipo tayari ishatumika mara 30, hakuna kitu kipya. Serikali ilegeze kidogo na kuwe na upatikanaji wa vibali kwa njia rahisi.

Una familia?
Nina mke na mtoto mmoja wa kiume, anaitwa Dayan.



Asante kwa ushirikiano wako.
Asante na wewe, karibu tenasiku nyingine.



SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic