April 11, 2016

MAYANJA
Kocha Mkuu wa Simba, Jackson Mayanja ameipigia hesabu kali mechi yake dhidi ya Coastal Union itakayochezwa leo Jumatatu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar kwa kuhakikisha wanashinda mchezo huo huku akifurahia kurejea kwa wachezaji wake nyota Hamisi Kiiza na Juuko Murshid waliokuwa katika majukumu ya kitaifa.

Coastal na Simba zitamenyana kwenye mchezo wa Kombe la FA katika hatua ya robo fainali, wakiwa wanawania kuingia hatua ya nusu fainali huku timu za Yanga, Azam na Mwadui zikiwa tayari zimeshaingia katika hatua hiyo.

Hata hivyo, Kiiza ndiye mshambuliaji pekee wa Simba aliyefanikiwa kuzifunga timu zote za Tanga msimu huu, hivyo kurejea kwake kunampa jeuri kocha huyo kuiondoa Coastal katika hatua hiyo.

Mayanja aliyewahi kuinoa timu hiyo amesema kikosi chake kipo fiti kuivaa Coastal leo huku wachezaji wake nyota wakiwa tayari wamesharejea kikosini.

“Nimejiandaa vyema na kikosi changu kuelekea mechi yetu na Coastal, tunahitaji kushinda mchezo huo ili kuweza kufanikiwa kuingia hatua inayofuata.


“Nashukuru wachezaji wangu wapo vyema na Kiiza na Juuko tayari wamesharejea kikosini na wanaendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo huo,” alisema Mayanja.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV