April 11, 2016


JUZI Jumamosi, Yanga ilikuwa na kibarua kigumu katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri, iliisha kwa sare ya bao 1-1.

Walioshuhudia watakiri kuwa haikuwa mechi rahisi kwa Yanga na inaonekana itakuwa ngumu zaidi katika mechi ya marudiano, hivyo lazima Yanga wajipange kwelikweli.
Jana, Azam FC timu nyingine ya Tanzania nayo ilikuwa na kibarua dhidi ya Waarabu wa Afrika Kaskazini. Hao ni Esperance kutoka Tunisia. Timu zote hizo mbili ni kubwa Afrika na mahiri katika michuano hiyo chini ya Caf, kwa ujumla si kazi ndogo.

Najua sasa angalau Watanzania wapenda michezo na hasa soka wanaanza ‘kulegeza’ mawazo yao na kufikiria mambo mengine kama hayo ya Yanga na Azam FC ikiwa ni baada ya wiki nzima ya mshangao na mshtuko.

Mshtuko wa kashfa nzito ya rushwa ambayo viongozi wa juu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanatuhumiwa kuhusika baada ya sauti zao kusikika wakipanga namna ya kuisaidia timu ya Geita Gold kupata matokeo mazuri, tena wanazihusisha taasisi nyingine za serikali, kwamba itoke Sh milioni 10 ipelekwe Idara ya Uhamiaji bado haujaisha.

Viongozi hao wanazungumza namna ambavyo fedha zinavyoweza kutolewa. Mmoja anajisifia kuacha kazi muhimu na kwenda kufanya kazi za rais. Mwingine akipanga fungu la fedha kwenda kwa viongozi wengine wa juu wa shirikisho hilo akiwemo katibu mkuu.

Wakati viongozi hao wanapanga hayo, tayari mmoja wao ametoa kauli yake na kusema sauti zao zimetengenezwa wakati mwingine ameendelea kuwa kimya na tayari kuna taarifa vyombo husika, vimeanza kulifanyia kazi.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), tumeelezwa imeshalichukua hilo na kuanza kulifanyia kazi na baadaye kipindi mwafaka baada ya kuwa wamelifanyia kazi, majibu yatatolewa.

Hakika si jambo la kuliacha lipite kwa kuwa Watanzania wanapaswa kupata uhakika wa hilo na mwisho kama majibu yatathibitisha basi hatua zichukuliwe.

Kwa wale ambao wanawajua viongozi wanaotuhumiwa, hakuna mjadala wa sauti kwamba zimetengenezwa na kuwaachia Takukuru wafanye kazi yao ni jambo zuri, lakini ukweli ndiyo huo.

Wakati Takukuru wakiendelea, vizuri Watanzania wanaopenda soka, wawe huru zaidi na huenda huu ndiyo wakati mzuri kabisa wawataje ambao wanawajua wamekuwa wakiwavuruga au wakitaka fedha ili kufanikisha jambo fulani.

Tumekuwa tunalia na waamuzi, tumekuwa tukisikia wachezaji fulani wamepanga matokeo jambo ambalo wote tunakubaliana ni baya na adui mkubwa katika maendeleo ya mpira kwa kuwa wahusika wameamua kuendeleza matumbo yao badala ya maendeleo ya jumla ya mchezo huo ambayo faida yake ni kwetu na taifa kwa ujumla.

Sasa tuhuma zimeingia ndani ya shirikisho. Vizuri zifanyiwe kazi kwa uhakika ili kujiridhisha na vizuri vyombo husika vinavyolifanyia kazi, vikalifanyia kazi kwa umakini na ufasaha mkubwa kwa kuwa yamekuwa ni maumivu makubwa kwa wapenda maendeleo ya mchezo huo.

Wengi wamekuwa wakiumia kutokana na rushwa na ubabe wa wanaochaguliwa ambao wengi wao wamejijengea ‘Umungu Mtu’ wakiona mpira ni mali yao, pia wakiamini Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) litawalinda. Lakini hata huko, waliokuwa wanaongoza rushwa, wamefumuliwa. Sasa ni zamu ya Tanzania.

Vizuri mjadala wa Yanga na Azam FC uendelee kuchukua nafasi. Lakini Watanzania lazima waendelee kukumbuka tuko katika kipindi cha mpito cha kutafuta dawa ya mpira wetu. Hivyo msisahau huku TFF kuna tuhuma ambazo kwa maana ya mwonekano wa kawaida, sisi tunaamini wahusika ni wenyewe na ndivyo inavyoonekana.

Lakini kwa maana ya uungwana na kufuata taratibu, Takukuru na wengine wanaoshughulikia, tuwape muda. Ingawa itakuwa vizuri nao wafanye kwa weledi, kasi na kuwapa Watanzania kilicho sahihi. Kila la kheri katika kufanikisha hili.0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV