April 2, 2016

MINGANGE...
Baada ya kuondolewa kwenye Kombe la FA na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, Kocha wa Ndanda FC ya Mtwara, Meja Mstaafu, Abdul Mingange amesema rafu ni tatizo kwenye kikosi chake.

Kauli hiyo, aliitoa baada ya kumalizika kwa mechi hiyo ya FA juzi Alhamisi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo Yanga ilishinda mabao 2-1.

Mingange aliyerudi kuifundisha Ndanda akitokea Mbeya City, amesema soka la rafu ndiyo lililowagharimu kutolewa kwenye hatua ya robo fainali ya FA.

Mingange alisema, wachezaji wake wanatakiwa kubadilika kwa kucheza soka la kisasa linalochezwa ulimwenguni kote na siyo soka la rafu ambalo lilisababisha wacheze pungufu baada ya Paul Ngalema kutolewa kwa kadi nyekundu.

Ngalema alimchezea rafu Simon Msuva wa Yanga na kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kisha nyekundu kwani awali alitenda kosa kama hilo na kuonywa kwa kadi ya njano. 

“Rafu ndizo zilizotuangusha na nitarekebisha hali hiyo, pia ni jambo la kushukuru kucheza na Yanga na kufungwa idadi hiyo ndogo ya mabao kwani wana kikosi bora kinachoongezeka ubora wakicheza taifa.

“Utaona kuna wakati tuliwashambulia sana na kupata matumaini ya ushindi lakini ndiyo soka, mambo hubadilika wakati mwingine,” alisema Mingange. 

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV