April 15, 2016



Na Saleh Ally
USIKU wa Jumanne, Azam TV walirusha moja kwa moja matangazo ya droo ya Kombe la Shirikisho linalodhaminiwa na Azam Sports HD.

Timu nne zimefanikiwa kuingia fainali ya kombe hilo zikiwa zinatokea katika mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Shinyanga na Tanga.

Matokeo ya droo hiyo iliyorushwa moja kwa moja yalionyesha hivi; Yanga itaanza kwa kuwa mgeni wa Coastal Union na mechi ya pili Mwadui FC itawakaribisha Azam FC kwao Shinyanga.

Suala la matokeo hayo, karibu kila mmoja alisifia kwa kuwa yalikuwa na uwazi. Hakuna timu iliyokuwa na malalamiko zaidi ya lile la Yanga na Azam FC kuomba mechi zao zisogezwe mbele kwa kuwa watakuwa na majukumu ya kimataifa na itakuwa ni siku chache baada ya kurejea wakitokea Tunisia na Misri ambako watakwenda kucheza na Esperance na Al Ahly. Hilo tuwaachie TFF.


Ukiingia kwenye mitandao mingi au gumzo kubwa katika sehemu mbalimbali ambazo zinahusisha wanamichezo ni namna Azam TV walivyoifanya droo hiyo moja kwa moja. Ni suala la maandalizi na lilivyoonekana.

Wapo wanaoamini kusema tu bila ya kutoa maoni au kueleza walichofikiri ndiyo jambo jema. Wapo wanaoamini kulaumu pekee ndiyo kuonekana wanajua sana.

Kueleza walichokosea ni vizuri, lakini kuwapongeza kwa walichoanzisha na kuwapa maoni ni kitu kizuri zaidi.


Hatuwezi kujua kama watapokea maoni au la lakini hatuwezi kukwepa kwamba kuwapa maoni ndiyo jambo sahihi ili waboreshe na mwakani wafanye jambo zuri zaidi ya hilo ambalo lilikuwa limefanyika.

Hata mimi niliona upungufu mwingi katika hilo lakini nimeweza kufikisha maoni yangu. Mfano, walipofanyia hakukuwa na mwanga wa kutosha, ilionekana hakukuwa na mazoezi kwa waliofanya na hasa mwalikwa Ester Chabruma ‘Lunyamila’ na hata vazi alilovaa, huenda angependa kuvaa na kuonyesha yuko kwenye shughuli ya usiku.


Hata waliokuwa na kamera hawakuwa tayari kutokana na kuvuta matukio. Mpangilio wa viti, utaona vilivyoonekana VIP viliwekwa nyuma na vilivyokuwa mbele vilikuwa vile vya mapokezi. Angalia karatasi zenye majina ya timu, zilikuwa kubwa wakati zingefaa ziwe ndogo halafu kamera ingezivuta ili msomaji aweze kuona.

Kuna ule mjadala kwamba hatua ya nusu fainali, michuano hiyo hakuna timu inacheza uwanja wake wa nyumbani. Badala yake ni ‘neutral ground’, lakini watu wamesahau kanuni za michuano hii si za ile ya England na huenda si wakati wake, lakini wana nafasi ya kuboresha na kuangalia wachukue mfumo huo au mwingine. Nafasi bado ipo.


Kwanza lazima Azam TV wakubali haikuwa imekaa vizuri katika maandalizi sahihi. Wanaokosoa, basi wawape maoni au mawazo chanya kwa ajili ya wao kujenga.

Kabla ya Azam TV, hakuna runinga iliyokuwa imefanya hivyo angalau kwa kiwango hicho hapa nyumbani. Ndiyo tunaanza kukua na michuano yenyewe ndiyo imeanza na huenda kuionyesha kwao moja kwa moja imechangia kufanya bora zaidi.

Utaona imekuwa na mwamko mkubwa kabisa. Kumbuka ilikuwa imekufa na sasa ni gumzo miongoni mwa wapenda soka.

Ukweli ni hivi; Azam TV wamejitahidi sana. Wameonyesha uzalendo na kinachotakiwa ni kuboresha mambo yote ambayo wameona yamepungua au kupunguza ubora.

Kufanya hivyo kutaifanya michuano hiyo kuwa bora zaidi na huenda maarufu au gumzo zaidi kuliko kombe jingine la FA kwa Afrika Mashariki na Kati.

SOURCE: CHAMPIONI 



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic