Mbuyu Twite na Haruna Niyonzima wamerejea mazoezini Yanga na kinachoonekana ni hivi, jambo hilo limeongeza faraja kwa Kocha Hans van der Pluijm katika maandalizi ya mechi ya pili dhidi ya Al Ahly ya Misri.
Yanga itapambana na Al Ahly, Aprili 19, mwaka huu huko Misri katika mchezo wa marudiano baada ya ule wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, kumalizika kwa sare ya 1-1.
Katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkubwa, Niyonzina na Twite walishindwa kuitumikia klabu yao kutokana na kuwa na matatizo mbalimbali.
Niyonzima alikuwa akiitumikia adhabu kutokana na kuwa na kadi mbili za njano alizozipata kwenye mechi mbili ambazo Yanga ilicheza dhidi ya APR ya Rwanda, wakati Twite alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa malaria.
Pluijm amesema kuwa kurejea kwa wachezaji hao uwanjani ni faraja kubwa kwake kwa sababu hivi sasa timu hiyo inakabiliwa na mechi nyingi muhimu ikiwemo ile ya marudiano na Al Ahly.
“Nimefurahi sana na ninamshukuru Mungu kwa hilo kwani hivi sasa tunakabiliwa na mechi nyingi ngumu, hivyo kurejea kwao kikosini kutasaidia kuwa na kikosi kipana kwa ajili ya kuhakikisha tunafanya vizuri,” alisema Pluijm.
0 COMMENTS:
Post a Comment