MAN CITY vs REAL MADRID, ATLETICO vs BAYERN MUNICH
Ratiba ya Nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya imepanga na
inavyoonekana shughuli itakuwa pevu.
Matajiri wa Jiji la Manchester, Manchester City wanatarajiwa
kukipiga dhidi ya Real Madrid wakati wabishi wa Jiji la Madrid, Atletico Madrid
watawavaa Bayern Munich.
Mechi za kwanza za hatua hiyo zinatarajiwa kuchezwa Aprili 26 na 27, mwaka huu kisha kurudiana Mei 3 na 4 ikiwa ni katika mchakato wa kuelekea kwenye fainali ya michuano hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa San Siro jijini Milan nchini Italia mnamo Mei 28, mwaka huu.
Real Madrid itakuwa ikiongozwa na safu ya ushambuliaji ya BBC inayoundwa na Gareth Bale, Karim Benzema na Cristiano Ronaldo anayeongoza kwa mabao katika michuano hiyo akiwa na mabao 16, hali ambayo inaifanya safu ya ulinzi ya Man City kuwa na shughuli pevu kuwazuia washambuliaji hao.
Man City yenyewe itahitaji straika wake msumbufu, Sergio Aguero kuwa kwenye ubora wa juu ili kuweza kuwavuruga Madrid ambao wanaonekana kuwa na hasira ya kuhitaji kulitwaa taji hilo kwa mara ya 11.
Aguero ni mzoefu wa mechi kubwa na pia siyo mgeni wa Rel Madrid kwa kuwa alishakutana nao mara kadhaa alipokuwa akiichezea Atletico Madrid.
Takwimu za nyuma zinaonyesha kuwa Man City na Madrid zimekutana mara mbili ambapo mechi ya kwanza Madrid ilishinda mabao 3-2 kisha ya pili ikamalizika kwa sare ya bao 1-1, mechi zote hizo zilichezwa msimu wa 2012/2013 katika michuano hiyohiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
0 COMMENTS:
Post a Comment