April 15, 2016

RAIS WA TFF, JAMAL MALINZI


Na Saleh Ally
NIANZE kwa kusema najua sana kama nawaudhi watu kuhusiana na kuzungumzia mara kwa mara kuhusiana na suala la sakata la kashfa ya rushwa ambayo sasa inafukuta kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambako viongozi wake wanatuhumiwa.

Najua wengi wasingependa kabisa kunisikia nikizungumza na ikiwezekana wasingependa kuona nipo naendelea. Bahati mbaya kwao, mimi nimeamua kuifanya kazi yangu kwa ufasaha, nitaendelea.

Najua Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) tayari imelichukua suala hilo na inafanya kazi yake kwa ubora kabisa.

Lazima tuwaamini Takukuru kwa kuwa wana wataalamu ambao wamekuwa wakiifanya kazi hiyo kwa muda mrefu, tena ni watu ambao wameisomea.

Ukiniambia niwashauri, basi nitawaambia wajitahidi kwenda kwa kasi nzuri ili Watanzania wapate majibu ya suala hilo ambalo binafsi naona liko wazi na wala halina kona hata kidogo.

Serikali ya awamu ya tano imebadilisha mengi, mambo hayaendi tena kwa mwendo wa kusuasua. Kila kitu kiko wazi na kwa kasi, umeona sehemu nyingi serikali imebadilisha mambo.

Hata upande wa michezo, chini ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, mambo yamekuwa yakienda vizuri, hakuna hadithi na anayeonekana ameharibu, basi mara moja hatua zinachukuliwa dhidi yake.

Hayo ndiyo matarajio yangu kutoka kwa Takukuru kwamba hakutakuwa na ‘kulala’ kwa mambo na badala yake ni kasi ya viwango vya uhakika. Najua kazi yenu ni ngumu, naheshimu hilo. Kila la kheri.

Wakati Takukuru wanaendelea na hili la tuhuma ya kashfa kubwa kabisa ndani ya TFF tokea kuanzishwa kwake, kwanza niwaonye wale wanaopambana kutaka kulizima suala hili.

Niwakumbushe hivi, kufanya hivyo ni kutaka kuendelea kuudidimiza mpira wa Tanzania na kuendelea kuwa sehemu ya walaji na wanaoshibisha matumbo yao lakini si kwa faida ya soka na Watanzania wote.

Kuendelea kufanya figisu, kuwatuliza watu, kuwabembeleza waache au waachane nalo au kuwatisha wale wanaotaka kuona mwisho wake ni kuonyesha kwa kiasi kikubwa kuwa nyie ni mnaoabudu rushwa, mnaowaunga mkono kwa nguvu rafiki zenu wala rushwa au mnajua kwamba wauaji wa soka ni kina nani na mmekuwa mkishirikiana nao.

Pamoja na hilo, pia ningependa niwashauri Takukuru, kwamba huu ndiyo wakati mzuri wa kufungua macho yao zaidi katika mchezo wa soka ambako rushwa ilikuwa kama halali.

Ligi Kuu Bara inakwenda mwishoni, Kombe la Shirikisho la Azam Sports HD pia linakwenda mwishoni. Huu ndiyo wakati wa kumulika zaidi upande huu wa wanamichezo.

Mwishoni mwa ligi ndiyo kipindi kikuu cha figisu, kipindi kikuu cha watu kubadilisha mambo kwa kutumia nguvu ya fedha badala ya uwezo wa soka uwanjani.

Huo ndiyo wakati ambao kuna watu fulani huamini kipindi chao cha mafanikio, kipindi cha kuona ‘maisha yanabadilika’ kimewadia. 

Wote wanaofikiria hivyo, ni wale wanaotaka kufaidisha na kufurahisha nafsi zao kwa kujiendeleza wao badala ya mpira huku wakiwa wamesahau, kama mpira utaendelea basi ‘automatically’ pia wataendelea tena zaidi ya namna wanavyoendekeza rushwa kwa sasa.

Rushwa haina tofauti na uzinzi, utasikia anayesifika kwa uzinzi sifa zinabaki juujuu kwa kuwa si rahisi kuona wakati anautekeleza na inakuwa rahisi sana kwake kusema anasingiziwa.

Ndivyo ilivyo katika suala la uchukuaji na upokeaji rushwa. Hatutakiwi kuwa wanafiki, lazima tukubali kwamba watu wanaochukua na kutoa rushwa wako wengi, wako kwa idadi kubwa na imekuwa ikipanda kila kukicha.

Kitu kibaya zaidi, kila siku zinavyosonga wanaona ni haki yao. Kwa yule ambaye anaeleza si jambo jema, ndiye anaonekana ni adui. Takukuru washeni taa nyingi zaidi, mmulike huku.0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV