April 18, 2016


Kila mbinu inapangwa sasa kwa ajili ya kuhakikisha kwenye mechi ya marudiano Yanga inaifunga Al Ahly ya Misri na kusonga mbele kwenye hatua ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika hilo, Kocha Mkuu wa Yanga, Mdachi, Hans van Der Pluijm, ameamua kubadili mfumo na kujaribu mfumo mpya kwa ajili ya kuhakikisha anawafumua Waarabu hao katika mchezo utakaopigwa Jumatano hii huko Alexandria, Misri.

Yanga iliyokuwa ikitumia mfumo wa 4-3-3 na 4-4-2, imeamua kubadili mwelekeo na kutumia 3-5-2 ambao iliujaribu kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa msimu huu katika mchezo wa juzi dhidi ya Mtibwa Sugar walioshinda bao 1-0.

Mfumo huu umekuwa ukitumiwa zaidi na Azam FC chini ya Muingereza, Stewart Hall na umekuwa ukiwapa matokeo mazuri, Pluijm yeye ameelezea kuhusiana na hilo huku akigusia kuwa, hayo ni maandalizi ya mechi yao hiyo ya kimataifa.

"Tumebadili mfumo kwenye mechi ya Mtibwa, tulijua tunakutana na timu yenye upinzani mkubwa, tulicheza 3-5-2 na tulikuwa na straika mmoja na bado tukatengeneza nafasi nyingi.

"Hii pia imekuwa kama sehemu ya maandalizi yetu kwa mchezo wa Al Ahly, tunaangalia vitu vingi na kubadili baadhi ya vitu kuelekea katika mchezo wetu huo. Upande wa utengenezaji nafasi ulikuwa mwingi lakini kama tungekuwa makini, tungefunga la pili na la tatu.

"Ukifunga mabao mengi na kucheza vizuri inasaidia kwa ajili ya maandalizi ya mchezo ulio mbele yetu, tunaendelea kufanyia kazi baadhi ya vitu," alisema Pluijm.

Katika mfumo huo, timu ikiwa inashambulia, Pluijm alitumia mabeki wa kati watatu, viungo watano na washambuliaji wawili, mmoja akifanya jukumu la kuunganisha timu kikamilifu kutoka kati kuelekea mbele.

Lakini timu ikiwa inakaba nyuma huongezeka na kuwa watano, viungo wanne na kumuacha mshambuliaji mmoja ambapo katika mechi ya juzi alitumika Donald Ngoma. 

Yanga iliyotarajiwa kuondoka jana Jumapili majira ya saa 10 kuelekea Misri, katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Al Ahly uliopigwa Uwanja wa Taifa, ilibanwa kwa sare ya bao 1-1.

Ili kusonga mbele, Yanga inahitaji ushindi wa bao 1-0 na zaidi au sare ya aina yoyote kuanzia 2-2 katika uwanja huo wa Alexandria.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic