May 11, 2016


Kiungo mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib Migomba anatarajia kuanza majaribio katika klabu ya Golden Arrows ya Afrika Kusini, kesho.

Tayari Ajib yuko jijini Durban ambako ni makao makuu ya klabu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1943.

Meneja wa Ajib, Juma Ndambile amesema mchezaji wake huyo atafanya majaribio katika kikosi cha Arrows kuanzia kesho.


“Kesho ndiyo siku anaanza majaribio, leo Arrows wana mechi. Kesho ndiyo ataungana nao na baada ya hapo tutaangalia nafasi nyingine,” alisema.

“Wakala wake amempa nafasi ya kufanya majaribio katika klabu nyingine ya daraja la kwanza ya Amazulu. Hii itakuwa ni baada ya Arrows kutoa majibu yao au wanaonaje,” alisema.

Ajib aliondoka nchini bila ruhusa ya uongozi wa Simba, inaelezwa Ndambile ndiye alimpigia simu Rais wa Simba, Evans Aveva kwamba mchezaji huyo anaondoka siku inayofuata.


Siku hiyo jioni, Ajib alikuwa amelambwa kadi nyekundu ya kujitakia wakati Simba ilipofungwa na Mwadui FC ya Shinyanga kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV