May 20, 2016Na Musa Mateja, Angola
NIANZE kwa kusema wazi kuna kila sababu kwa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), kuzitupia macho nchi kama Angola hasa inapofikia timu zinazoshiriki michuano fulani, zinakuwa zinacheza nje ya Jiji la Luanda.

Unakumbuka Januari 7, 2010 ule mkasa wa basi la wachezaji wa timu ya taifa ya Togo kushambuliwa katika eneo la Cabinda ambako si mbali sana na eneo la Dundo.
Nilikuwa Dundo ambako nilifika pale baada ya safari ndefu kabisa ambayo ilikuwa na lengo moja tu. Kwangu ni kuripoti matukio wakati Yanga ikipambana na Sagrada Esperanca ya Angola.

MATEJA
Ilikuwa mechi ya Kombe la Shirikisho na Yanga walifika Angola wakiwa na faida ya mabao 2-0 waliyoyapata jijini Dar es Salaam.

Safari ilikuwa ni kupitia Afrika Kusini ambako tuliunganisha ndege hadi Luanda. Hapo ndipo kazi ilipoanza na figisu za kila aina. Kama kweli mpira ni fitna, basi hawa jamaa wamezidi.


Kwanza hawakutaka hata kuzungumza na viongozi wa Yanga. Watu wa uwanjani walionyesha ujeuri wa kupindukia. Baadhi ya watu tulioongozana na timu tukalazimika kulala Luanda baada ya kupatikana kwa ndege ambayo ilitosha kuwabeba wachezaji.

Siku iliyofuata, tukaanza safari nyingine ndefu. Moja, tulipanda ndege kwa saa mbili hadi Lucapa ambako ndiyo kuna uwanja wa ndege. Baada ya hapo ikaanza safari nyingine ya zaidi ya kilomita 100 kufika Dundo.

Tayari wachezaji wa Yanga walikuwa wamefika salama Dundo pamoja na mikasa kadhaa ikiwa ni pamoja na kuharibikiwa gari wakiwa njiani.

Kilichonishangaza baada ya kuwa Dundo, ni baadhi ya maofisa mbalimbali wa timu hiyo waliosema wako upande wa ulinzi kusisitiza hawataruhusu wapigapicha.

Nilipohoji sababu, walisema kuwa wanafanya hivyo kwa kuwa waandishi wao walinyanyaswa walipokuwa jijini Dar es Salaam na kukatazwa kupiga picha. Nikawakatalia kata kwa kuwa baadhi ya waandishi waliokuja Dar es Salaam wakiwa na Esperanca nilikuwa nao karibu wakati tukipiga picha kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Kama haitoshi, mmoja wao alipoteza kitambulisho na nikamsaidia kukipata. Baada ya kuwapa maelezo hayo wakaonekana kupoa kidogo.

Baadaye wakaondoka, halafu wakarudi tena na kusema kwamba bado msimamo wao ni uleule. Kwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alikuwa karibu, aliwasikia. Akaamua kuingilia na kuwaelekeza hata shirikisho la soka la nchi hiyo liliwapa ruhusa ya kupiga picha lakini si video.

Baada ya mzozo huo, kidogo walionekana kuelewa. Mimi niliwaeleza ofisini, nilizungumza na bosi wangu, Saleh Ally ambaye alinieleza kushirikiana na Sanga katika hilo.

Kweli Sanga alinipa ushirikiano mzuri, nikalala nikiamini hakuna tatizo. Siku ya mechi, nilifanikiwa kuingia uwanjani. Lakini ajabu, nikakataliwa kuingia ndani ya uwanja sehemu ambayo ningepiga picha na baadaye wakaja walinzi na kunitoa nje nikiwa na mwandishi mwingine, Gift Macha.

Nilishangazwa sana na hilo, msisitizo ulikuwa tusione mechi. Mwisho Sanga alikuja na kwa pamoja tukashirikiana naye kupinga hilo. Baada ya mzozo mkubwa na kusukumana, walikubali tuingie ndani lakini hatukutakiwa kukaa uwanjani na badala yake na kamera yangu wakasema nipande juu jukwaani.

Sikuwa na la kufanya, kwa kuwa ofisini walinipa kamera ya kazi, (kama zile unazoziona wanatumia The Sun, Daily Mail, Marca au kwenye Ligi Kuu England, Kombe la Dunia na kadhalika). Hivyo sikuwa na wasiwasi wa kukosa picha.
Nikiwa pale jukwaani, Saleh Ally alinipigia na kunipa maelekezo.

“Hakikisha unapiga picha haraka, halafu zitume kwenye e-mail ya ofisini haraka. Najua hawatakuacha hivihivi, watarudi na ikiwezekana watakupokonya kamera.
“Pia unaweza kupiga picha, tuma halafu toa hiyo kadi uihifadhi na uweke mpya ambayo ni ndogo,” alisema.

Kweli nilifanya hivyo, ile ninamaliza tu kutuma picha. Jamaa hawa hapa, wakaanza kunipokonya kamera jukwaani. Ukawa mzozo, mmoja wao akanikaba kama anataka kunitoa roho.

Halikuwa jambo zuri, hata kama walitaka kuidhulumu Yanga lakini bado walitakiwa kuniacha nifanye kazi yangu. Hakika nilisafiri kutoka mbali lakini bado waliendeleza manyanyaso zaidi.

Kamera walichukua, nafikiri walipekua na kurudisha na hawakuambulia kitu kwakuwa nilishafanya ‘umafia’.
Hata baada ya mechi, waandishi na wachezaji wa Yanga tulitolewa uwanjani kwa tahadhari kubwa. Mashabiki walitusubiri watupige, kosa lilikuwa lipi?

Tulipofika hotelini tukakuta jezi, sare za Yanga zimeibwa. Mshambuliaji mpole, Amissi Tambwe alikuwa ameibiwa simu. Hakika ni sehemu ya watu wa ajabu hivi.
Hii kweli ni Dundo, akili zao ni uonevu na kutaka kudunda tu. Hawafai kabisa na Caf inapaswa kuzitupia macho sehemu za hovyo kama hizi. Sitarudi tena Dundo.

SALEHJEMBE


1 COMMENTS:

  1. kaka pole sana kwa masaibu yaliyokufika pamoja na timu nzima ya Yanga,hakika mpira si ujiranio mwema tena bali ni vita.najua kabisa CAF hawatafanya lolote kwa mataifa makubwa yenye pesa kwani ndio wanaowaingizia mamilioni kila mwaka,laiti ingekuwa ni TZ imefanya hivyo basi rungu lingetuangukia.Na ndio sababu timu zetu za Africa hazifanyi la maana katika makombe ya dunia kwani tunaenda huko kwa figisu x2 tuu.

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV