Na Saleh Ally
IMEKUWA ni kawaida kabisa kusikia timu fulani inafanya usajili wa mbwembwe na sisi vyombo vya habari tukaandika kuelezea namna ambavyo timu fulani imempata mchezaji mpya kutoka nchi fulani.
Vyombo vya habari vimekuwa vikilaumiwa, kwamba vinawapamba wachezaji. Lakini ukweli havifanyi usajili na wahuosika ndiyo wanaojua kuhusiana na wachezaji hao.
Kueleza huko nyuma walivyofanya kupitia rekodi zao, si jambo baya. Ndiyo maana wapo ambao wamekuwa wakipingwa kutokana na walivyo kwa maana ya rekodi au pale wanapoanza kucheza.
Klabu zimekuwa zikifanya usajili wa wachezaji kutoka ndani na nje ya Tanzania. Mara nyingi, zile zinazofanya usajili wa wachezaji wa nje zinakuwa na uwezo wa juu kifedha.
Mara nyingi hazizidi sita, mfano kwa timu za jeshi zenyewe zaidi zinasajili wachezaji wa nyumbani. Yanga, Simba, Azam FC na nyingine chache angalau zinakuwa na uwezo wa kusajili wachezaji wa nje.
Kusajili mchezaji wa ndani au wa nje linaweza lisiwe jambo muhimu sana hata kama litakuwa na ukubwa wa namna gani. Lakini muhimu ni mchango wa wale wanaosajiliwa wakati ligi itakapoanza.
Katika suala la usajili, wote tunajua kuwa suala la mgawo au ujanjaujanja wa watu kushibisha matumbo yao, haliishi.
Wapo ambao wanausubiri msimu wa usajili kama sehemu ya kufaidika kimaisha. Hata kidogo hawaangalii hasara kwa klabu husika hapo baadaye ili mradi wao watakuwa wamesogeza kidogo chao mfukoni.
Wapo baadhi ni viongozi, wapo baadhi ni watu wa pembeni ambao wapo karibu na klabu hizo. Wanaamini huu ni wakati wa neema kwa sasa lakini umekuwa ni mateso kwa klabu pale ligi inapoendelea.
Inakuwa ni mateso kwa kuwa mchezaji aliyesajiliwa anakuwa hana uwezo mzuri na anageuka kuwa mzigo wakati analipwa fedha nyingi kuliko hata wazalendo ambao wanakuwa msaada kwa timu.
Mchezaji wa kimataifa anasajiliwa, anaanza kucheza akiwa benchi na wakati mwingine kuingia dakika za mwishoni huku akiwa analipwa mshahara wa juu, kapangiwa nyumba bora na hii inachangia mara nyingi kushusha morali ya timu kuliko hata kusaidia suala la mafanikio.
Mchezaji wa kigeni anapitishwa kiujanja na hili wakati mwingine linatia hofu kwa makocha wa timu husika kwamba wanaweza vipi kukubali wachezaji ambao wanaona hawana msaada kwa vikosi vyao?
Wanakuwa wanawaogopa viongozi wao? Au nao huwa wanapozwa na kuachia mambo yaende ilimradi na watajua namna ya kuziba mapengo hapo baadaye?
Kwangu naona suala hili la usajili, kila linapofika kunakuwa na mtandao mkubwa ambao hujitakia njia ya kula au kujiingizia fedha, hivyo unapita na ndiyo maana wachezaji wasio na uwezo sahihi kutoka nje ya nchi wamejazana nchini.
Wachezaji kutoka nje ambao uwezo wao ni ule wa saizi ya chini hadi ya kati, wapo hapa nchini na hawana msaada katika timu zao zaidi ya kusaidia majungu tu kwa kuwa wana uwezo mdogo na wanapokosa nafasi ya kucheza basi wanajenga vikundi vya majungu ili wapate nafasi zao za visingizo.
Utaona wachezaji wenye misaada na timu zao, hakuna anayeweza kufumbua mdomo na kulaumu. Inaonekana kazi wanayoifanya na ubora wake. Inawezekana wote wanaweza wasiwe na ubora unaofanana, lakini wengine uwezo wao uko chini ya wazawa. Sasa faida yao nini hapa nchini zaidi ya kuchota fedha ambazo wangepewa wazalendo ambao wana uwezo wa kufanya vizuri zaidi yao?
Hao wanaogawana asilimia 10 au ten percent kama ilivyo maarufu ndiyo wamekuwa tatizo kubwa kwa kuwa wengi wao wana nguvu ndani ya klabu hizo, hivyo wanaitumia kuwapa nafasi hata wenye uwezo wa chini wasajiliwe na mwisho ni hasara kwa klabu wakati wao wanaendelea kusherehekea riziki hiyo haramu.
Wakati mzuri ni huu, klabu zijipime, ziachane na kubebewa kila kitu, badala yake kila kitu kiende kitaalamu zaidi na makocha muache woga, la sivyo mtaingia kwenye kipande cha ten percent.
0 COMMENTS:
Post a Comment