Real Madrid imetinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itakayochezwa Mei 28 katika jiji la Milan nchini Italia.
Madrid imetinga fainali hiyo ikiwa ni ya 17 kwake na imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mara 10 ambayo ni mara nyingi zaidi kuwahi kuchukuliwa na timu yoyote ya Ulaya.
Wakati Madrid inatinga fainali hiyo leo, jana wapinzani wake wakubwa na hasimu namba moja kwao Atletico Madrid, walitinga fainali wakiing'oa Bayern Munich inayofundishwa na Pep Guardiola.
Licha ya ushindi wa mabao 2-1, lakini Bayern imeshindwa kuwazuia Atletico Madrid ambao wamefuzu kwa bao la ugenini lililofungwa na Antoine Griezmann.
Sasa ni derby ya Madrid nchini Hispania inakwenda kuchezwa katika ardhi ya Italia huku kukiwa na kumbukumbu ya miaka michache tu kuhusiana na derby of Madrid kuchezwa kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mwaka 2014, Madrid ilibeba ubingwa wa Ulaya kwa kuifunga Atletico Madrid katika fainali, mechi ilichezwa Lisbon, Ureno. Atletico imerejea fainali ikiwa na kocha wake yuleyule, yaani Diego Simeone lakini Madrid imetinga fainali ikiwa na Zinadine Zidane. Wakati ule ilikuwa chini ya Carlo Ancelotti.
Mwaka huo, Madrid ilitinga fainali kwa kuing'oa Bayern Munich na Atletico ikaiondoa Chelsea. Mwisho Madrid wakawa mabingwa baada ya kupata bao dakika za mwisho lililolazimisha mpira kwenda dakika 30 zaidi. Mwisho Madrid ikafanikiwa kushinda kwa mabao 4-1.
Katika nusu fainali, timu mbili za hispania ziliingia ambazo ni Madrid na Atletico huku England ikiingiza timu moja, Manchester City na Bayern Munich kutoka Ujerumani. Mwisho timu zilizotinga fainali zote ni kutoka Hispania.
Hii inaonyesha muendelezo wa timu kutoka Hispania kuendelea kufanya vizuri katika michuano mikubwa ya Ulaya.
0 COMMENTS:
Post a Comment