GAO AKISALIMIANA NA WACHEZAJI WA TOTO AMBAO ANAWAPENDA ZAIDI WACHEZAJI WA YANGA KULIKO HAO AMBAO YEYE NI MAKAMU MWENYEKITI!!! |
Na Saleh Ally
MAKAMU Mwenyekiti wa Toto Africans ya Mwanza, anaitwa Waziri Gao.
Gao ni mkazi wa Jiji la Mwanza, shabiki mkubwa wa Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara na wenye nafasi kwa asilimia 95 hadi sasa kuutwaa ubingwa huo na ilivyo inaonekana hakuna wa kuwazuia tena.
Kiongozi huyo wa juu aliyechaguliwa na wanachama wa Toto Africans baada ya kufanya kampeni bora, ni shabiki wa kutupa na mwenye uchungu wa juu kabisa kwa Yanga.
Mapenzi ya Gao kwa Yanga ni makubwa kuliko yale ya Toto. Uchungu kama Yanga ikiumizwa, maumivu kwa Gao ni makubwa zaidi kuliko ikitokea hivyo kwa Toto.
Kwa hali hiyo ya Gao, unategemea kweli Toto inaweza ikapiga hatua vipi wakati anayeiongoza anaipenda timu nyingine kuliko yenyewe? Kwanza acha nikukumbushe kidogo kuhusiana na Gao.
Gao amesimamishwa na Kamati ya Utendaji ya Toto baada ya uamuzi wake wa kujiengua na kusema anaipenda Yanga kuliko Toto, hiyo ilikuwa ni siku chache kabla ya timu hizo kukutana katika mchezo muhimu wa Ligi Kuu Bara uliokuwa unatarajiwa kupigwa jijini Mwanza.
Gao aliamini kama Yanga ingefungwa, basi inaweza kupoteza nafasi ya ubingwa. Akaamua kuomba akae pembeni hadi mechi hiyo itakapopita, halafu atarejea kwa kuwa anaipenda Yanga zaidi!
Uongozi ukamkubalia, lakini baada ya kupumzika kwake, ukaona unapaswa kumjadili na mwisho ukapitisha uamuzi wa kumsimamisha.
GAO MWENYEWE HUYO... |
Gao anahoji kuhusiana na suala la yeye kusimamishwa huku akisema katiba ya Toto ambayo bado iko kwa msajili haisemi lolote kuhusiana na hilo, kwamba ukiongoza Toto hauruhusiwi kuipenda timu nyingine!
Hilo tu ndiyo linazidi kunipa hisia za wazi kwamba timu nyingi za mikoani hazitaendelea kwa kuwa viongozi wengi wanaoziongoza timu hizo ni wale wanaozipenda Yanga na Simba.
Kama Gao kasema, kabla ya kusema alifanya mangapi, lakini Gao unayeweza kumpongeza kwa kusema, unajua wangapi ambao wamekaa kimya wanaiongoza Toto na moyo wao ni ‘mali ya Yanga’?
Haushangazwi na kusikia kiongozi hajui kama kuingoza timu fulani huku ukiipenda nyingine tena zilizo katika mashindano yaleyale ni kitu cha ajabu kabisa! Nani anaweza kuniambia katika timu za mikoani akina Gao wangapi?
Kwangu nafuta kuanzia leo kwamba timu za mikoani zitabadilika na kurejesha utamaduni wa ushindani uliowahi kutokea kwa timu za mikoani kutwaa ubingwa wa Bara na ule wa Muungano kama walivyowahi kufanya Coastal Union ya Tanga, Mecco ya Mbeya na Majimaji ya Songea.
Watu kama Gao ndani ya klabu za mikoani ni kama sumu. Gao hakupaswa kuingoza Toto, badala yake alipaswa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Yanga Tawi la Mwanza au ‘kokote kule’. Angefanya hivyo angesaidia maendeleo ya Yanga ambayo anaipenda.
Kuongoza kitu usichokipenda hakika ni kupoteza muda na kubabaisha mambo. Unaweza kusema anayefanya hivyo zaidi anajali sifa, mbinafsi au ni mwenye njaa. Vipi uwe ndani ya Toto na utamani Yanga kuifunga timu yako?
Gao anawezaje akakaa pembeni asiingilie chochote wakati angependa Yanga iifunge Toto na yeye ndani ya klabu hiyo ana marafiki na watu wanaomheshimu? Ambao akiamua ana uwezo wa kuwashawishi.
GAO AKIWA NA KOCHA WA TOTO, JOHN TEGETE, VIONGOZI WENGINE PAMOJA NA WADAU |
Kuna jambo kubwa na muhimu sana kujifunza katika suala hili la Gao. Pia kwa viongozi walio ndani ya uongozi wa timu nyingi lazima wengi watakuwa na mapenzi ya Yanga na Simba. Huu ndiyo wakati wa kubadilika na kuachana na ujinga wa kuamini kila mpenda mpira lazima atakuwa anaipenda Yanga au Simba, imepitwa na wakati.
Huwezi kusema kiongozi wa Leicester City anatamani Manchester United au Liverpool ishinde dhidi ya timu yake. Viongozi wake wanaipenda timu hiyo, wanataka ishinde na kufanikiwa, ndiyo maana wamefanikiwa kuwa mabingwa. Hili ni somo kubwa na zaidi ya lile unalolijua.
Kina Gao mliojificha mjitokeze, njooni hadharani muwe wakweli ili tuusaidie mpira wa Tanzania. Wanaozipenda timu hizo na wenye nia ya kuzipa maendeleo ndiyo wapewe nafasi.
Mimi nafikiri GAO angekuwa mpenzi wa Simba wala hasingeondolewa katika kiti chake na wewe Saleh usingeleta huu ujinga hapa mezani!
ReplyDelete