May 4, 2016
Na Saleh Ally
DAKTARI  wa kiitaliano Giuliano Poser ndiye aliyeelezwa kuwa mlinzi bora zaidi wa afya ya mshambuliaji hatari kuliko wote duniani kwa kipindi hiki.

Lionel Messi raia wa Argentina ndiye tumaini kubwa la Barcelona kuhakikisha wanabeba ubingwa wa Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ kwa mara nyingine.

Kwa mwendo ambao wamekuwa wakienda nao, Barcelona bado wako katika kipindi kigumu kwani wakati ligi imebakiza mechi mbili kwisha kwa kila timu, Barcelona ina pointi 85 kileleni sawa na Atletico Madrid katika nafasi ya pili, lakini bado Real Madrid katika nafasi ya tatu ina piinti 84.

Ubingwa wa La Liga unaweza kuchukuliwa na timu yoyote kati ya hizo tatu. Barcelona imebakiza mechi zote mbili nyumbani na inachotakiwa ni kushinda zote.


Atletico, pia Madrid zina mechi moja nyumbani, moja ugenini. Nazo zitatakiwa kushinda mechi zote mbili na kuomba ‘njaa’ kwa Barcelona.

Wakati inaonekana Barcelona inatakiwa kushinda mechi hizo mbili, tumaini kuu linabaki kuwa Messi ambaye kwa msaada mkubwa wa daktari Poser anaonekana kuwa amepungua kilo tatu.

Amepungua kilo hizo tatu baada ya kutakiwa kupunguza kula vitu vya sukari nyingi kama pipi, chocolate. Pia alimzuia kula vyakula vyenye wanga mwingi hali kadhalika mafuta na alimtengenezea utaratibu wa kitaalamu wa mlo, au ‘dayat’ bora.

Wakati daktari huyo kutoka Italia akifanya hivyo kuhakikisha Messi anafanya vema na kuisaidia Barcelona kutwaa ubingwa. Mimi nikakumbuka maneno niliyoelezwa na mmoja wa waandishi wa gazeti la Marca lenye makao makuu yake jijini Madrid.


Kidogo nilishangazwa na aina ya uchezaji wa Messi, kwamba kasi yake imepungua. Hisia zangu ilikuwa ni hivi; huenda Messi ameridhika sana na mafanikio. Maana niliona akicheza kama ‘faza’ fulani hivi.

Pablo Polo, anasema Messi hayuko fiti asilimia 100. Barcelona wamekuwa wakisumbuka kumuacha amalize msimu huu ili awe na maandalizi ya msimu ujao.

“Majeruhi mfululizo yamempa wakati mgumu sana, alitakiwa kupumzika muda mwingi zaidi. Lakini Barcelona wameona wanamhitaji naye anahitaji kuisaidia.

“Kilichofanyika ni kuhakikisha anacheza hadi mwisho wa msimu. Wakaangalia njia sahihi ya kufanya na ndiyo kinachofanyika sasa hivi. Utaona Messi anacheza kama mtu asiye na haraka, lakini anatakiwa kukimbia kilomita kadhaa na si kama zamani.

“Utaona wamemrudisha nyuma kupunguza hatari. Anacheza katikati zaidi na yeye sasa kazi yake kubwa ni kuchezesha timu na si kufunga ingawa ikitokea anafanya hivyo.

“Kucheza katikati anapunguza hatari ya kukutana na mabeki ambao wanaaminika kila unaposogelea eneo la 18, wanazidi kuwa wakatili kwa kuwa hawataki kufungwa,” anasimulia mwandishi huyo.


“Kuna wakati, daktari anamkumbusha Messi mambo kadhaa. Mfano hakuna haja ya kukaa sana na mpira au asikimbie sana.”

Barcelona inajua athari za kucheza bila Messi, inawezekana wangefanya vizuri lakini wanajua watainua morali ya wapinzani wakigundua hatokuwepo.

Ingawa ni siri, bado inaonekana kibiashara kwa klabu na kwake, kukaa nje mwezi mmoja na zaidi si sahihi. Badala yake kilichofanyika ni njia mbadala ili acheze na ndiyo maana yametokea hayo ya kubadilishwa namba na kubadilishwa aina ya uchezaji.

Pamoja na hivyo, kumekuwa na taarifa ambazo si rasmi, kwamba Barcelona waliwasilisha maombi rasmi La Liga, kuhakikisha waamuzi wanaongeza ulinzi kwa Messi ambaye amekuwa ni mhanga wa viatu vya mabeki wakatili.


Hakuna ubishi kwamba kiufungaji Messi ameporomoka. Lakini Barcelona wanajua namna wanavyoweza kushughulika na hilo.
Wanautaka ubingwa, lakini wako makini kuhakikisha wanakuwa na Messi sahihi msimu ujao.

Huenda hapa kuna kitu cha kujifunza, namna ambavyo klabu inavyoweza kujali kupata ubingwa lakini ikaonyesha kwa kiasi gani inaweza kumthamini mchezaji wake kwa kumuwekea mikakati imara awe msaada kwao lakini awe salama pia kiafya.

Kwa mwendo ulivyo, La Liga bado ngumu na haina mwenyewe. Lakini uwepo wa Messi katika dakika 180 za Barcelona uwanjani. Hakika ni faida maradufu na uhakika wa juu wao kuweza kufanikiwa kuwa mabingwa tena ambao watafuta machozi baada ya kung’olewa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

TAKWIMU:
BARCELONA
Mei 8:
Barcelona Vs Espanyol
Mei 15:
Barcelona Vs Sevilla

ATLETICO
Mei 8:
Levante Vs Atletico Madrid
Mei 15:
Atletico Madrid Vs Celta Vigo

MADRID
Mei 8:
Madrid Vs Valencia
Mei 15:
Derpotivo Vs Madrid


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV