May 4, 2016


Na Saleh Ally
AZAM FC ni kati ya timu ambazo zimeingia kwenye historia ya soka nchini, kwamba ni moja ya zile zilizowahi kubeba ubingwa wa Tanzania Bara.

Kikosi cha Azam FC chini ya Kocha Joseph Omog, raia wa Cameroon, kilibeba ubingwa wa Tanzania Bara kwa msimu wa 2013-14.

Azam FC imekuwa ikishika nafasi ya pili mara tatu, unaweza kusema kuwa wanastahili kuitwa moja ya timu zinazojitahidi sana.

Timu ya Azam FC, kwa kiasi kikubwa inaonekana imeleta mabadiliko na sasa ni kati ya zile zinazoweza kuitwa kubwa katika soka hapa nyumbani.

Baada ya Yanga na Simba, ilikuwa ni lazima uitaje Mtibwa Sugar hasa baada ya wakongwe wengi kama Majimaji, Coastal Union, African Sports na wengine ‘kupotea njia’.


Pamoja na mwendo wa Azam FC, bado kwangu mimi naweza kutofautiana na watu wengi sana. Pongezi zitakuwepo, lakini ninachoona wachezaji wengi wa Azam FC bado hawajitambui kama inavyostahili kuwa.

Tangu Azam FC imetwaa ubingwa 2014, imeendelea kubaki katika nafasi ya pili. Hakika si jambo baya, ingawa msisitizo wangu unaendelea kubaki palepale kwamba wachezaji Azam FC, bado hawajatenda haki kwa waajiri wao.

Naendelea kukubali kwamba wanafanya vizuri, lakini walistahili kufanya vizuri zaidi kulingana na mazingira waliyopo ambayo yanatengenezwa na mwajiri ambaye ni makini.

Azam FC wanalipwa vizuri zaidi, wana kiwanja kizuri zaidi cha mazoezi. Ndiyo timu pekee yenye kiwanja bora zaidi cha nyumbani.

Kama utazungumzia vifaa bora kabisa vya mazoezi vya mchezo wa soka nchi hii na ikiwezekana Afrika Mashariki, vinapatikana Azam FC. Umeona wachezaji wanafanya mazoezi na ‘parachut’, wachezaji wanaingia katika mapipa ya barafu.


Azam FC ndiyo timu pekee ina mtaalamu wa masuala ya chakula. Huenda kwa Afrika Mashariki na Kati ni TP Mazembe pekee wanaweza kuwa na hilo.

Angalia mchezaji wa Azam FC anapoumia, wamekuwa wakisafirishwa kwenda kupata matibabu ya uhakika nje ya nchi. Hivyo hakuna anayeweza kuwa na hofu ya kujituma.

Ukisema hata usafiri, huenda wachezaji wa Azam FC wanaongoza kwa kupanda ndege. Hata wanaposafiri na barabara, basi lao ndilo bora kuliko jingine lolote, angalau kidogo Gor Mahia ya Kenya wanaweza kujifananisha nao.

Lakini mara nyingi sana nimeona mechi ambazo huwezi kutofautisha kiwango cha Azam FC inapokutana na JKT Ruvu au wanapokutana na Ndanda, Mgambo au timu nyingine za Ligi Kuu Bara ambazo maisha yao yamekuwa ni ya kuunga au kawaida tu.


Ninaamini kabisa, huenda wachezaji wa Azam FC kama walivyo binadamu wengine, wamejisahau mapema kwa vigezo tofauti. Wapo wanaoamini ndiyo “wenye timu” au wakaona wamefika bila ya kujua akili ya mwajiri ni mafanikio, hivyo siku moja anaweza kubadilika ghafla kama akiona anachoshwa na nafasi ya pili, kutoka mapema katika michuano ya kimataifa.

Naendelea kusisitiza, Azam FC haifanyi vibaya. Lakini ninaamini wanachofanya, bado wanastahili kufanya zaidi ya hapo hasa kama wataona utofauti walionao dhidi ya wengine na mwajiri wao anavyojitoa kwao.

Anayejitoa kwako, utamlipa kwa kujitoa kwake na hakuna kingine. Muhimu zaidi wanapaswa kukumbuka kazi ya kucheza mpira na kuipa timu mafanikio makubwa ni yao, mwajiri amekuwa akitimiza yake kwa ufasaha mkubwa.


Kama wachezaji wa Azam FC watahakikisha wanaondoa hisia za rekodi na historia za Yanga na Simba, basi watakuwa na uwezo wa kuleta mabadiliko na kufungua ukurasa wa mfalme mpya anayefuatiwa na wakongwe.

3 COMMENTS:

 1. Azam wanasikitisha,ht ukiangalia kasi waloanzanayo inapungua kila siku, hawana spirit ya tim km vile wanacheza kujivua lawama.
  Kwa upande wangu nadhan kocha wao kashindwa kuwajenga fikra za uzalendo ili wacheze kwa manufaa ya tim,mfano mzuri ni Yanga walifungwa na Waarabu na wachezaji wakalia inaonesha waliifia tim,angalia Yanga wanavyoongeza kasi ya kutafta ushindi km wakiwa wametangulia kufungwa,ni tofaut na Azam wenye kila kitu kinachotakiwa ktk mpira.

  ReplyDelete
 2. ni kweli kabisa mwandishi, nimeangalia mechi yao majuzi na simba, walikosa umakini kabisa, walikuwa wanakosa magoli ya wazi kabisa utafikiri hawana mazoezi ya kutosha, mchezaji kama singano alikuwa tishio sana na msumbufu kwa mabeki, lakini sasa hivi kiwango chake sio kizuri kabisa (ingawa bado anacheza vizuri)anakabika kabisa, juzi ilifikia kipindi walimfanyia sub

  ReplyDelete
 3. AZAM NI TIMU YA KAWAIDA SANA, BAHATI MBAYA sIMBA INA MATATIZO YA UONGOZI LAKINI WANA TIMU NZURI ZAIDI YA OVERATTED AZAM FC

  ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV