May 23, 2016


Bado kocha wa zamani wa Simba, Mserbia, Milovan Cirkovic, anaendelea kufukuzia ajira ya kukinoa kikosi cha Wekundu hao msimu ujao baada ya kuibuka na maombi mapya kwa uongozi wa timu hiyo.

Milovan ambaye ndiye kocha wa mwisho kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara timu hiyo mwaka 2012, aliondoka kikosini hapo msimu wa 2012/13, baada ya kufanya vibaya kwenye mechi 13 za mzunguko wa kwanza na nafasi yake kuchukuliwa na Mfaransa, Patrick Liewig.

Hata hivyo, tangu wakati huo Milovan amekuwa mtu wa kuifuatilia Simba mwenendo wake na amekuwa akiulizia ajira mara kwa mara kwa ajili ya kuja kuinyanyua timu hiyo.
Habari za ndani ya Simba zimeeleza mchakati wa makocha unaendelea.

“Milovan amerudi tena lakini inakuwa ngumu kidogo kumchukua kwa sababu wajumbe wengi wameonekana kutofurahishwa na kurejea kwake kikosini, ana nafasi ndogo sana ya kutua hapa. Nafikiri ataangaliwa kocha mwingine,” kilisema chanzo hicho.


Pamoja na hayo, awali ilielezwa kuwa Simba ingempa nafasi Bobby Williamson, raia wa Scotland aliyewahi kuinoa Gor Mahia ya Kenya na timu za taifa za Uganda na Kenya lakini bado kuna mvutano baina ya wajumbe kuhusiana na kutua kwa kocha huyo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV