May 13, 2016


Na Saleh Ally
INAWEZEKANA kabisa bila ya ubishi ni mateso makubwa kuwa shabiki wa timu ya Simba kwa kipindi hiki.

Mashabiki wa Simba wanaumia kwa kuwa hawana kile wanachokitaka, wanakitafuta lakini hawajakipata na kabla ya kukipata, wengine wamekipata na wanaendelea kukipata.

Huu ni msimu wa nne sasa, Simba haijashiriki michuano ya kimataifa. Lazima ukumbuke Simba ni timu yenye sifa hiyo, kushiriki na kufanya vizuri nje ya Tanzania.

Rekodi zinaibeba kwenye mambo mengi sana. Timu ambayo imefanya vizuri zaidi kwa ukanda wa Afrika Mashariki katika michuano ya ukanda huo kwa kuwa wamechukua mara nyingi zaidi.

Bado rekodi zinaibeba Simba Afrika. Ndiyo timu pekee ya Tanzania kufikia fainali ya michuano mikubwa zaidi kwa upande wa klabu. Hii ni kwa Afrika Mashariki yote, wao ndiyo pekee wamecheza fainali ya Kombe la Caf mwaka 2003.

Kwa miaka hii minne, miwili wakati wa uongozi wa Ismail Aden Rage na miwili chini ya Evans Aveva, Simba imefeli na imewafanya baadhi ya Wanasimba kuona kwamba mambo sasa yameshindikana.
Miaka minne bila ya mafanikio hata kidogo. Awali ilionekana Simba imeteleza tu, msimu wa pili ikaonekana itajirekebisha. Wa tatu, utakuwa wa mwisho na sasa ni wanne, mwisho wa haya utakuwa baada ya muda gani?

Aveva aliichukua Simba kwa Rage ikiwa imechoka kwa misimu miwili mfululizo. Mategemeo ilikuwa ni kurekebisha, sasa ni misimu miwili tena, mambo ni yaleyale.

Huenda huu ni wakati mzuri Wanasimba wakaanza kutafakari na kupata majibu ambayo yatakuwa sahihi kwa ajili ya wao kubadili gia. Kweli wamefeli misimu minne bila ya mafanikio hata kidogo.

Hata iwe vipi, lazima tukubali, Simba kufeli kwa misimu minne si jambo dogo hata kidogo. Simba si Ndanda wa JKT, kila mmoja anaujua ukubwa wake kama ambavyo nilianza kuelezea.
Kama kweli vipindi vizuri vimeyeyuka na vile vigumu vimeendelea mfululizo huku vikiendelea kutanua mioyo ya Wanasimba kwa maumivu. Wao ndiyo watakuwa waamuzi wazuri wa njia sahihi ya kupita.

Inawezekana kabisa wakafanya maamuzi ya hasira au kukomoana, ukawa ni wakati wa kujiangusha pia kutengeneza njia nyingine ya kuendelea kuumia kwa miaka mingine nane. Ikiwezekana ikafikia siku na kusema: “Huu ni mwaka wa nane, Simba bado haijabeba kombe wala kushiriki kimataifa”.

Wakati kunapokuwa na tatizo, inawezekana mkafanya uamuzi fulani ambao lazima muupime na kujua utakuwa unaleta matokeo ya kuharibu zaidi au kusaidia. Umakini wa juu unahitajika hapa.

Ushauri wangu, uongozi wa Simba ufikie wakati sasa ukubali kila ulipokosea na kuanza kurekebisha, lakini kuna kila sababu ya kukutana na wanachama ndani ya siku kadhaa baada ya ligi kwisha.

Wanachama ndiyo wenye timu, wapewe nafasi ya kutoa dukuduku. Uongozi upokee na kukaa kuangalia yaliyo sahihi, uyafanyie kazi kwa manufaa ya klabu hiyo. Baada ya hapo waanze tena, mwisho watachanganya.

Lakini kwa wale wanaotaka uongozi kwa udi na uvumba, basi wanapaswa kukumbuka maana ya maslahi ya Simba. Tamaa yao ya madaraka isiiangushe Simba kwa miaka mingine minne. Wafikirie kwamba kuiangusha kabisa, ni kujitwika mzigo baadaye hata wakipata nafasi ya kuiongoza.

Hakuna asiyejua, viongozi wakitaka madaraka, basi huangalia maslahi yao kwa maana ya kutaka kushinda hata kama wanaanzisha kitu ambacho kitaanzisha chuki au kuporomoka kwa jambo muhimu la klabu.


Huu ni wakati mzuri wa kuangalia maslahi ya klabu yenu kwanza. Vizuri muungane na kushirikiana, baada ya hapo mengine yatafuatia. 

Hakika, kama Simba iendelee hivi tena, basi wa kulaumiwa watakuwa Wanasimba wenyewe, kuanzia viongozi, makocha, wachezaji lakini hata wanachama. Hapa ninatia msisitizo, wakati huu ni wa kuelezana ukweli, kuwa na moyo wa kweli wa mapenzi ya klabu na sahauni ubinafsi. Mliokosea mkubali kuelezwa na kurekebisha, msipofuata haya, mtavuruga zaidi ya hapa. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic