May 13, 2016



Na Saleh Ally
MFUNGAJI bora wa Ligi Kuu Tanzania mwaka 2004 alikuwa kijana Abubakar Mkangwa kutoka jijini Dar es Salaam, lakini wakati huo anakipiga katika kikosi cha Mtibwa Sugar.

Mkangwa hakuwa na mbwembwe nyingi, lakini mwepesi, fundi na mjuzi. Msimu uliofuata Isse Abshir ‘Ronaldo wa Somalia” akaifungia Simba mabao 16 na kuwa mfungaji bora wa 2005.

Hawa wawili, hakuna aliyekuwa amefikisha mabao 20 hadi mwaka 2006, Abdallah Juma wa Mtibwa Sugar alipofunga idadi hiyo. Juma alikuwa mshambuliaji mtaratibu, asiye na makeke uwanjani kama ilivyokuwa kwa Mkangwa na Abshir. Mpira ukitua, anaugusisha nyavu, anakimbilia kwenye kibendera.

ABDALLAH JUMA (KATIKATI) AKIPAMBANA NA MABEKI WA SIMBA, AMRI SAID 'STAM' NA BONIFACE PAWASA.
Tangu Juma aliyekuwa mshambuliaji asiye na ladha kumuona machoni, maana hakuwa na mbwembwe, achana na mavazi ya mbwembwe nje ya uwanja, hata anapoitumikia Mtibwa Sugar, ilikuwa ni nadra kuona amepiga chenga au kuwatoa mabeki watatu. Kikubwa kwake ni nafasi, kazi imeisha.


Tangu Abdallah Juma afunge mabao hayo 20 mwaka 2006, hakuna mshambuliaji au kiungo mwingine awe mwenyeji au mgeni anayecheza katika timu ya Ligi Kuu Bara, aliyefanikiwa kuifikia rekodi hiyo.

Hadi mabadiliko yanafanyika kutoka katika ligi inayochezwa kwa mwaka mmoja, hadi ile ya nusu mwaka na mwaka mwingine. Hakuna aliyefanikiwa kufikisha idadi zaidi ya mabao 19.

Msimu wa 2007-08, ilichezwa ligi ndogo ikiwa ni kipindi cha mpito kwenda kuingia kwenye mfumo mpya. Mganda Michael Katende wa Kagera Sugar akaibuka na zawadi ya mfungaji bora, akiwa amefunga mabao 11 tu.

Baada ya hapo, mfumo wa msimu ukaanza kutumika na mshambuliaji wa kwanza kuwa mfungaji bora katika mfumo wa msimu ni Mkenya, Boniface Ambani wa Yanga aliyepachika nyavuni mabao 18.


Mrundi Amissi Tambwe amevunja rekodi ya Abdallah Juma aliyekuwa wa mwisho kufunga mabao hayo 20 ndani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Tambwe ameweka rekodi ya kuwa mgeni wa kwanza kufunga zaidi ya mabao 20 kwa wachezaji wa kigeni waliocheza Tanzania.

Pia ameweka rekodi mpya ya kuwa mchezaji mwenye mabao mengi zaidi Ligi Kuu Bara ndani ya kipindi cha misimu mitatu tu baada ya kufunga mabao 54.

Msimu wa 2013-14, aliibuka mfungaji bora akiwa ametua Simba kwa mara ya kwanza anatokea Vital’O ya Burundi ambako pia alikuwa mfungaji bora wa Burundi na mfungaji Bora wa Afrika Mashariki na Kati.

Msimu uliofuata, akahamia Yanga akiwa na bao moja na kufunga mengine 13, mwisho akawa na mabao 14 akishika nafasi ya pili nyuma ya Simon Msuva aliyefunga 17.

Msimu huu, bado kuna mechi mbili. Anafukuzana na Hamisi Kiiza wa Simba mwenye mabao 19, akiwa amefunga mengi zaidi kwake kwa mara ya kwanza.


Bado Tambwe hajawa mfungaji bora kwa kuwa Kiiza naye ana nafasi za kubadilisha mambo katika mechi hizo mbili kama kweli atacheza, lakini hadi sasa, tayari Tambwe amevunja rekodi ya Abdallah Juma iliyokaa kwa miaka 10 bila ya kufikiwa au kuvunjwa na wageni au wazalendo.

Tambwe ameifikia na kuivunja rekodi hiyo ndani ya wiki moja. Bao lake la 20 alifunga wakati Yanga ikicheza dhidi ya Stand United mjini Shinyanga. Halafu akaivunja rekodi hiyo kwa kufunga bao la 21 akicheza dhidi ya Mbeya City.

Furaha kubwa kwa Tambwe, pamoja na kuvunja rekodi hiyo, bao lake la 21 lina nafasi kubwa ya kuwa bao bora la msimu. Kwani alilifunga akiwa nje ya 18 baada ya kumchungulia kipa wa Mbeya City, Juma Kaseja na kufunga kwa ufundi wa juu kabisa.

Tambwe anafanana kwa kiasi kikubwa na Abdallah Juma. Hii inaonyesha washambuliaji wa aina hiyo wanaweza kuwa hatari zaidi ya wengine.

Abdallah Juma hakuwa mtu wa mambo mengi ndani na nje ya uwanja. Hasa kama utazungumzia vilevi. Uwanjani hakuwa mtu wa makeke, yeye alichotaka ni kukaa kwenye nafasi na kufunga.


Rekodi hiyo iliwekwa naye miaka 10 iliyopita, aliyeivunja pia si mtu wa mambo mengi. Hana makeke nje na ndani ya uwanja. Hataki “vyenga”, badala yake anakaa kwenye nafasi, anatikisa nyavu.

Utaona hawa wawili ni mgeni na mzalengo lakini wanarandana kwa mambo mengi muhimu na yanaonyesha ni sehemu ya vigezo bora kwa wafungaji bora.




TAKWIMU:
2004
Abubakar Mkangwa (Mtibwa Sugar) 16

2005
Isse Abshir (Simba) 19

2006
Abdallah Juma (Mtibwa Sugar) 20

 2007-08
Michael Katende (Kagera) 11

 2008-09
Boniface Ambani (Yanga) 18

2009-10
Mussa Mgosi (Simba) 18

 2010/11
Mrisho Ngassa (Azam) 18

2011/12
1. Bocco  (Azam)                   19
2. Emmanuel Okwi (Simba)    12
3. Nsa Job (Villa)                   12
4. Mutesa Mafisango (Simba)   11
5. Hamisi Kiiza (Yanga)           10 


2012/13
1. Kipre Tchetche (Azam)        17         
2. Dider Kavumbagu (Yanga)    10         
3. Paul Nonga (Oljoro)              9         
4. Jerry Tegete (Yanga)            8          
5. Themi Felix (Kagera)            8

 2013/14
1. Amiss Tambwe (Simba)           19         
2. Kipre Tchetche       (Azam)     13         
3. Mrisho Ngassa (Yanga)            13         
4. Elius Maguri    (Ruvu)             13         
5. Hamis Kiiza      (Yanga)          12         


2014/15
1. Simon Msuva  (Yanga)                  17   
2. Amissi Tambwe  (Yanga)              14  
3. Abasrim Chidiebere        (Stand)   11  
4. Emmanuel Okwi       (Simba)         10  
5. Didier Kavumbagu     (Azam)         10



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic