May 13, 2016

BAADHI YA WASHINDI WA MAJIMAJI SELEBUKA MWAKA JANA
Mambo safi kuelekea katika tamasha la kila mwaka la Majimaji Selebuka 2016 litakalofanyika Mei 28 hadi Juni 4, mwaka huu, habari njema kwa washiriki upande wa mashindano ya mbio za baiskeli ni kuwa kuna shavu la kwenda Rwanda kwa ajili ya kupata mafunzo ya mchezo huo ngazi ya kimataifa. 

Tamasha hilo litakalofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji mjini Songea, Rukwa litakuwa la aina yake kutokana na ushiriki wa mataifa mbalimbali ambayo yamethibitisha ushiriki wake.

Hata hivyo ‘bahati ya mtende’ kwa Watanzania ni kwamba washindi watatu watapata ofa ya kwenda kupata mafunzo ya kimataifa ya mchezo huo mbali na tuzo watakazojinyakulia kwenye tamasha.

Mratibu wa tamasha hilo, Reinafrida Rwezaura amesema: “Hii ni ofa kwa Watanzania tu watakaoshiriki. Haijalishi wamalize katika Tatu Bora ama la, cha msingi tutaangalia kwa upande wa Watanzania wa kwanza mpaka wa tatu, hao watakwenda Rwanda kwa mafunzo ya siku 10 kama sehemu ya kukuza na kuibua vipaji na kuendeleza michezo nchini.”

Mbali na baiskeli, pia kutakuwa na michezo kama Mashindano ya Ngoma za Asili, riadha kwa mbio ndefu na fupi, maonyesho ya biashara kwa wajasiriamali pamoja na shughuli za kijamii kama utalii wa ndani, midahalo kwa shule za sekondari na mengine mengi.

Aidha, Reinafrida aliomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki, ikiwa ni mara ya pili kufanyika kwa tamasha hilo ambalo lilianza kuratibiwa mwaka jana na kuacha gumzo kwa mwitikio mkubwa wa wananchi.0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV