May 7, 2016Kocha wa Azam, Stewart Hall, amesema bado yupo Azam FC lakini anachoshwa na mambo yanayofanywa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na hayo yanaweza kuwa sababu ya yeye kuacha kazi.

Hall alisema hayo baada ya TFF kuipoka Azam pointi tatu kutokana na kumtumia Erasto Nyoni katika mchezo wao dhidi ya Mbeya City wakati ana kadi tatu za njano. 

Hall raia wa Uingereza amesema mambo mengi yamekuwa yakifanywa na TFF ambayo hapendezwi nayo kwani yanarudisha nyuma maendeleo ya soka nchini.

Alisema kwa sasa anachokiangalia ni kuona namna gani anaipa ubingwa wa Kombe la FA timu yake na kumaliza Ligi Kuu Bara katika nafasi ya pili, na baada ya hapo ataangalia mustakabali wake kama abaki au la.

 “Si wachezaji wala makocha wanaorudisha nyuma soka la Tanzania, bali TFF ndiyo watu wa kulaumiwa kwani wamekuwa wakifanya uamuzi ambao si sahihi, wanakandamiza baadhi ya watu na timu zao.


“Nimekuwa nikiwalalamikia sana, lakini kwa sasa naona bora nikae kimya na mwisho wa msimu huu nitaamua kama nitaendelea kubaki hapa au niondoke,” alisema Hall.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV