May 7, 2016


Na Saleh Ally
UNAWEZA ukajiuliza kwani hawa Waingereza kutokea England wako wapi? Tatizo lao ni lipi hasa, maana hawaonekani tena Ulaya!

Miaka mitano hadi kumi iliyopita, ilikuwa ni kitu cha kawaida kabisa kusikia Timu ya Hispania au Italia ina mchezaji kutoka England ambaye anafanya vizuri na timu hiyo.

Lakini safari hii katika michuano ya Ulaya kuanzia msimu uliopita inaonekana wachezaji kutoka England wamekuwa wakipotea katika timu mbalimbali zinazofanya vizuri Ulaya.

Ajabu zaidi, hadi katika timu zinazotokea England, bado hakuna nafasi kwa wachezaji wanaotokea England hata kama timu zao zitafanya vizuri.


Mfano mzuri ni huu, ukichukua timu nne zilizoingia nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, utaona namna wachezaji kutoka England wanavyozidi kupotea kwa maana ya ubora linapofikia suala la ubora katika Bara la Ulaya.

Timu ya kwanza ni Bayern Munich ya Ujerumani ambayo haina mchezaji hata mmoja kutoka England. Kikosi hicho kimejaza Wajerumani, Wahispania, Wafaransa, Wabrazil na wengine kutoka Uholanzi, Poland, Chile na kwingineko.

Hatua ya nusu fainali ni Top Four ya Ulaya. Timu nyingine iliyoingia ilikuwa ni Atletico Madrid, nayo haina hata mchezaji mmoja kutoka England. Badala yake Wahispania ni wengi zaidi wakifuatiwa na Wabrazil, Waargentina, pia kutoka katika mataifa ya Ureno, Ghana, Slovenia na mengineyo.


Timu ya tatu ni Real Madrid, hawa pia hawana mchezaji anayetokea England. Isipokuwa wana mchezaji kutoka Uingereza. Huenda ninaweza kufafanua kidogo hapa.

Wales ni sehemu ya Uingereza kama ilivyo England. Kawaida England imekuwa ndiyo inatamba zaidi kwa ubora wa soka katika muunganiko wa nchi za Uingereza yaani Great Britain.

Madrid zaidi ina wachezaji kutoka mataifa ya Hispania, Ureno, Ufaransa, Croatia, Wales, Ujerumani, Colombia na Costa Rica.


Sasa labda twende kwa timu ya nne, hii ni Manchester City ya England. Ilijitahidi sana ingawa imetolewa hatua hiyo ambayo ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufika.

Man City katika kikosi chake cha timu ya wakubwa ina wachezaji wanne tu kutoka England ambao ni Joe Hart, Richard Wright, Fabian Delph na Raheem Sterling.

Katika wachezaji hao watatu, katika mechi za Ligi ya Mabingwa mwenye uhakika wa kuanza alikuwa mmoja tu, Hart ambaye ni kipa na angalau Sterling amekuwa akipata nafasi ya kuingia.

Lakini Wright ambaye ni kipa na kiungo Delph, hawa maisha yao yalikuwa ni nje ya uwanja.


Timu inayotokea England, ni mmoja tu tokea England mwenye uhakika wa kuanza tena ni kipa! Wako wapi wachezaji kutoka nchi hiyo inayoelezwa ni nyumbani kwa soka?

Angalia Man City, katika mechi zake za Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa asilimia 95 inategemea wachezaji kutoka katika nchi za Argentina, Ufaransa, Hispania, Ubelgiji, Brazil, Ivory Coast, Nigeria na kwingineko? Majigambo ya watu hawa yako wapi na wapi walipokosea?

Wakati wakina David Beckham, Michael Owen, Steve McManamann walifanya vizuri wakiwa Madrid ambayo ilikuwa na wachezaji nyota kabisa duniani kama Zinedine Zidane na Ronaldo na wakaonyesha ushindani.

Sasa hakuna wachezaji bora wanaotokea England wenye uwezo wa juu wa kushindana na wachezaji kutokea Hispania, Ufaransa na kwingineko duniani.

Waingereza wakiwa kwao walikuwa wakitamba zaidi na mfano mzuri ni Wayne Rooney. Ikaonekana wanaibuka akina Danny Welbeck na wengineo lakini sasa wote wamepotea. Vijana na walioonekana ni wakongwe.

Inaonekana England imepoteza mwelekeo na sasa inaanza kutengeneza mastaa wapya kama akina Harry Kane, Jamie Vardy na wengine wachache. Lakini hauwezi kusema ina wachezaji wa kiwango cha juu duniani ambao unaweza kusikia wanawaniwa na Real Madrid au Barcelona.

Lakini bado katika timu nyingi kubwa ni nadra kusikia mchezaji wa England ni tishio na gumzo hadi nje ya England. Sasa hakuna ubishi tena kuwa England na  Uingereza kwa ujumla wanatakiwa kufanya kazi ya ziada ili warejee juu katika soka la dunia, la sivyo wataingia kwenye hofu ya kupotea katika heshima ya ubora wa juu kisoka kama ilivyo hofu ya kupotea kwa vifaru kwenye mbuga za wanyama. Maana England hawapo England, hawapo Ulaya!


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV