May 7, 2016

Uongozi wa Toto African umesema utawachukulia hatua kali wachezaji wake wawili tegemeo Athumani Miraji na Hamad Waziri ambao walitoweka katika timu kabla ya kucheza na Yanga.

Miraji ambaye ni kiungo mshambuliaji na Hamad ambaye ni kiungo, wote wanadaiwa na uongozi wao kuwa walitoroka kambini na kwenda kusikojulikana kabla ya mechi na Yanga na hawajarudi hadi sasa.

Katika mchezo huo uliochezwa hivi karibuni, Yanga ilishinda mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na kuzusha hali ya sintofahamu ndani ya kikosi cha Toto Africans.

Kamati ya Utendaji ya Toto imetoa uamuzi huo kufuatia tuhuma mbalimbali zilizojitokeza kabla na baada ya mchezo dhidi ya Yanga, ikisema kutoroka kwa wachezaji ni sababu ya timu yao kufungwa. 

Ofisa Habari wa Toto, Carthibert Japhet amesema kitendo cha wachezaji hao waliowahi kuchezea timu ya vijana ya Simba, kuondoka kambini bila kutoa taarifa kwa uongozi ni uvunjaji wa sheria na kanuni zilizo kwenye mikataba yao. 

“Tunawatafuta wachezaji wetu wawili ambao ni Athumani Miraji na Hamad Waziri, wachezaji hawa walitoroka kambini siku chache kabla ya mechi na Yanga kitu ambacho ni utovu wa nidhamu.

“Kwa kuwa bado wana mikataba na Toto, kamati imekubaliana kuwatafuta na kuwapa adhabu kali ikiwemo kuwafungia pindi watakapopatikana ili iwe fundisho kwa wachezaji wengine,” alisema Japhet.


Nahodha wa Toto, Hassan Khatib alithibitisha kutoweka kwa wachezaji hao na kuongeza; “Sijui walipo, inaonekana wana tatizo na uongozi.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV