May 4, 2016


Huku Yanga wenyewe wakisubiria Ligi Kuu Bara imalizike ili wafanikishe usajili wa beki wa kulia wa Simba, Hassan Kessy, sasa sakata hilo limekuwa kama filamu ya kusisimua baada ya Azam jana kumteka na kumalizana naye kwa asilimia kubwa kuhusu usajili wake.

Beki huyo, hivi sasa ameziingiza kwenye vita kubwa Yanga inayofundishwa na Mholanzi, Hans van Der Pluijm na Azam iliyo chini ya Muingereza, Stewart Hall, zote zikimuwania.
Kessy ni mchezaji huru hivi sasa anayeruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine yoyote itakayomhitaji kwa ajili ya msimu ujao kutokana na mkataba wake kumalizika mwezi huu mwishoni.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa Azam, beki huyo Jumamosi iliyopita alipigiwa simu na viongozi wa timu hiyo kwa ajili ya kwenda kukutana naye na lengo likiwa ni kufikia makubaliano ya dau la fedha analolihitaji na mahitaji yake mengine ikiwemo nyumba ya kuishi na usafiri.

Chanzo hicho kilisema, uongozi wa Azam umefikia makubaliano hayo ya kumsajili kwa ajili ya kuongezea nguvu safu yao ya ulinzi hasa pembeni, hiyo ni baada ya beki wao, Shomari Kapombe kusumbuliwa na majeraha ambayo yamemsababishia kushindwa kumalizia mechi za mwishoni za msimu huu.

Kiliongeza kuwa, beki huyo jana alitarajiwa kutua jijini Dar es Salaam akitokea Morogoro alipokwenda kupumzika akitumikia adhabu ya kutocheza mechi tano za ligi kuu baada ya uongozi wa Simba kumfungia kwa kosa la kumchezea rafu mshambuliaji wa Toto Africans, Edward Christopher na kupewa kadi nyekundu.

“Kessy leo (jana) anatarajiwa kukutana na viongozi wa Azam kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kumsajili kwa ajili ya msimu ujao, wameanza naye mazungumzo ya mapema kwa ajili ya kuiwahi Yanga inayomhitaji.
“Viongozi walizipata taarifa za Yanga kumuwania Kessy kwenye usajili wao katika msimu ujao, hivyo uongozi umeona ni vyema ukaanza mchakato huo mapema wa kumsajili.

“Kessy atawasili Dar asubuhi (jana) akitokea Morogoro na mara baada ya kumalizana naye, basi atarudi huko kwa ajili ya mapumziko,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa Kessy kuzungumzia hilo alisema: “Hizo taarifa za mimi kupigiwa simu na viongozi wa Azam umezipata wapi? Naomba nisilizungumzie hilo suala kwa kipindi hiki, tusubirie kwanza ligi imalizike kwani kila kitu kitajulikana.

“Mimi hivi sasa bado mchezaji wa Simba hadi ligi kuu itakapomalizika, na wao ndio wanaopaswa kunilipa mshahara hadi sasa, hivyo nisingependa kuongea kitu chochote kwa hivi sasa,” alisema Kessy.

SOURCE: CHAMPIONI 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic