June 6, 2016
Na Saleh Ally
NAJUA tabia za Watanzania ni kuoneana haya tukiamini kumueleza mtu ukweli ni sawa na kumuumiza. Lakini ukweli ni dawa na nguzo kubwa katika kubadili mambo au kutafuta maendeleo.

Huu ndiyo wakati mwafaka wa Kocha Charles Boniface Mkwasa, kukaa kando na Taifa Stars iangalie utaratibu mpya.

Nakumbuka, niliwahi kumnunulia zawadi Mkwasa, akaniita mbele ya wachezaji na kunishukuru, hii ilikuwa nchini Uturuki. Lilikuwa jambo jema ambalo ninalikumbuka hadi leo, nilifanya hivyo kwa uzalendo wangu, Mkwasa akanionyesha ukomavu wake, lakini hapa sasa tunajadili suala la utaifa.

Bado nakumbuka, mara baada ya Mkwasa kuchukua nafasi kutoka kwa Kocha Mart Nooij aliyefeli kuliko wote Stars, nilikuwa mmoja kati ya niliochangia kuhakikisha mzalendo anapewa ushirikiano kwa kuwa tumejaribu sana kwa wageni bila ya mafanikio.


Hakuna anayeweza kukataa tena kwamba hata Mkwasa hakuna mabadiliko makubwa aliyoyafanya pamoja na matatizo yetu. Taifa Stars sasa iko nje ya michuano ya Kombe la Mataifa Afrika na pia nje ya michuano ya Kombe la Dunia.

Hakuna tena Stars chini yake ambacho inaweza kupata zaidi ya mechi moja ya ‘kirafiki’ dhidi ya Nigeria ikiwa ni ya kukamilisha ratiba.

Rekodi ya Mkwasa ni kuifundisha Taifa Stars mechi tisa, ameshinda moja, sare nne na amepoteza mechi nne.

Ninaweza nikakueleza kwa nini ninasema huu ni wakati wa Mkwasa kuondoka. Ninaona wachezaji tulionao, bado wana nafasi ya kutusaidia kupiga hatua, lakini kwa uwezo wa Mkwasa huenda tusifike mbali sana.

Hiki ni kipindi cha kuangalia kocha mwenye rekodi bora zaidi ikiwezekana katika michuano ya Afrika au zaidi ili aweze kuwasaidia tulionao kufanya jambo kubwa zaidi.

Kumuacha Mkwasa tena, ni kuendelea kujaribu kwa mara nyingine. Mkwasa ameonyesha alipofikia ndiyo mwisho, utaona inaonyesha wazi hakuna kipya ambacho anaweza kufanya, vizuri tukampa mkono wa shukrani na kocha mwingine mwenye uwezo wa juu ambaye tunaweza kuweka matumaini yetu kwake, akapewa nafasi.


Angalia mechi hizi nne za Waarabu, nianze na zile za kuwania Kombe la Dunia dhidi ya Algeria, Stars imefungwa mabao 9 katika mechi mbili. Yenyewe ikafunga mabao mawili tu.

Hizi mbili za kuwania Kombe la Mataifa Afrika dhidi ya Misri, Stars imefungwa mabao sita na yenyewa ikafunga moja. Hiki ni kipimo kinachoonyesha namna gani tunapaswa kufanya mabadiliko na kocha bora zaidi ya Mkwasa anaweza kuwa chachu kwa wachezaji kufanya bora zaidi.

Mkono wa Mkwasa umekuna alipofikia, ndiyo maana unaona hata katika mechi kati ya Stars dhidi ya Misri alishindwa kuamini mapema kwamba baada ya dakika 45 za mwanzo, beki Haji Mwinyi alipaswa kupumzishwa, tena huenda alipaswa kupumzishwa hata kabla ya mapumziko kwa kuwa hakuwa vizuri.

Au unaweza kushangazwa vipi aliamua kumpanga Mwinyi aliyetokea katika kipindi cha majeruhi, akawa amecheza mechi chache kabisa za ligi ukilinganisha na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye amekuwa katika kiwango bora kwa muda sasa na hakuwa akipata nafasi katika kikosi chake kucheza licha ya kumuita mara kwa mara.

Kati yetu, hakuna anayeweza kumdharau Mkwasa kwa kuwa kweli amejitahidi au kujitutumua kufanya vema. Hili ni jambo jema na nembo nzuri kwa makocha wazalendo na wanapaswa kujiamini hivyo.


Lakini mshale sasa unasoma tofauti, kwamba anapaswa kuachia ngazi au kutoa nafasi kwa kocha mwenye uwezo wa juu zaidi ambaye ataanza mapema kazi na kikosi cha Stars kukijenga ili tutakaporejea mashindanoni, basi kuwe na uhakika.

Kumbakiza Mkwasa, maana yake mwaka mmoja au miwili ijayo tuendelee kuwa na hesabu kama za miaka miwili iliyopita. Tutaendelea kuchelewa kila kunapokucha.
Tumejaribu sana bila ya kuchoka, najua tutaendelea. Lakini Mkwasa anapaswa kuwa sehemu ya majaribio au kupambana huko lakini katika kitabu cha historia. Halafu nahodha mpya wa jahazi, akabidhiwe kocha mwenye ubora wa juu zaidi yake.

Kigezo cha uzalendo, bado hakitoshi kwa Watanzania kuacha Mkwasa aendelee kubaki wakati dira inatuambia alipofikia, ndiyo mwisho wake.

Ili ufanikiwa Afrika lazima uwe na kikosi imara na kocha bora mwenye uwezo wa kupambana na nguvu za uwezo wa soka la Afrika Kaskazini na Magharibi. Hawa ndiyo wanaotawala.

Nirudie kidogo, rekodi ya Mkwasa inaonyesha hivi, mechi za mashindano na zile za kirafiki zikiwemo za kirafiki mazoezi kama ile ya Libya, jumla ameiongoza Stars kwa mechi tisa na ameshinda moja tu huku akipoteza nne na sare nne. Kumbuka, hata mechi za kirafiki, hakuna hata moja aliyoshinda.


Stars chini yake imeshinda mechi moja tu dhidi ya timu ya Chad ambayo ni ugenini. Hii ni sehemu tosha ambayo ni takwimu ambazo zinaonyesha juhudi za Mkwasa zinaweza kuthaminiwa na baada ya hapo apewe nafasi ya kusonga mbele ili tuendelee na utaratibu mwingine na yeye kama mzalendo kwa kuwa yupo, anaweza kuwa anatoa ushirikiano kila utakapohitajika kwa kocha atakayepewa nafasi.


Huu ni ushahidi kuwa, kama tunataka kwenda haraka, basi mwenye uwezo zaidi apewe, kikosi kiwe imara kupitia kocha huyo bora. Tukiendelea kuoneana haya, tutabaki tulipo. Anayetafuta kawaida hachoki, hongera Mkwasa na kila la kheri.

 REKODI ZA MKWASA STARS
Amecheza: Mechi 9
Ameshinda: 1
Ametoka sare: 4
Amefungwa: 4


MECHI;
Chan
Uganda 1 vs 1 Tanzania

Afcon
Tanzania 0 vs 0 Nigeria

Mechi ya kirafiki
Tanzania 1-2 Libya

Kufuzu Kombe la Dunia
Tanzania 2 vs 2 Algeria

Mechi ya kirafiki
Tanzania 1-2 Afrika Kusini

Kufuzu Kombe la Dunia 
Algeria 7 vs 0 Tanzania

Afcon 
Chad 0 vs 1 Tanzania


Mechi ya kirafiki
Kenya 1 vs 1 Tanzania

Afcon
Tanzania 0 vs 0 Misri
0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV