June 6, 2016


Na Saleh Ally
MOJA kwa moja nianze kuwakumbusha wachezaji wa kigeni wanaotaka kuja kucheza hapa nyumbani Tanzania, kwamba tunahitaji viwango sahihi na si mambo ya ubabaishaji.

Pia ninakwenda moja kwa moja kuwakumbusha kwamba, Tanzania ni nchi yenye vitu vingi ambavyo unaweza kuvipima kwa kiwango cha juu kuliko hata nchi nyingi za jirani zikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia na nyingine nyingi.

Hapa, ninazungumzia suala la malipo, ushabiki wa soka ulio na nguvu na ikiwezekana hata maisha bora kwa wachezaji wa kigeni wanaokuwa hapa nyumbani Tanzania.

Nimeanza kuwaeleza ambacho wanataka Watanzania lakini kuwakumbusha ubora wa Tanzania maana kuna wachezaji wengi wamekuwa wakijisahau baada ya kufika nchini kwa kuanza kujiona wao ni bora na wanatokea katika nchi bora kuliko Tanzania jambo ambalo si kweli hata kidogo.

Namshukuru Mwenyezi Mungu nimefanikiwa kufika nchi nyingi, hizo nilizozitaja na nyingine nyingi barani Afrika, hivyo nitakuwa nikizungumza kwa mifano sahihi na si ile ya kufikiri au mawazo tu.Wachezaji kutoka Uganda, kwangu wanakuwa mfano wa kwanza, wako wameweza kuonyesha viwango na wengine wamekuwa mizigo mikubwa.

Wako wachache walioonyesha viwango lakini wakataka kujigeuza wao wafalme na baadaye kuanza kuwadharau wachezaji wengine wa Tanzania, jambo ambalo limekuwa likinishangaza kwa kuwa wanapotokea hapawezi kulingana na Tanzania hata kidogo.

Najua msisitizo wa ujio wa wageni, wazawa wanapaswa kuwaheshimu. Lakini wageni wanapaswa kuonyesha heshima ya juu na Tanzania maana kwa wakati husika, ndiyo inawapa maisha.

Lakini zaidi wanapaswa kukumbuka, wanapokuwa hapa ni kazini na timu za Tanzania zinasajili wageni si kwa sura zao, majina ya nchi zao au mwendo wao badala yake wanataka ubora ambao unaweza kuzaa ushindani utakaosaidia kupatikana kwa mabadiliko katika maendeleo ya soka nchini.

Klabu zinapaswa kuwa na kipimo sahihi cha uchezaji wa wageni walio hapa nchini badala ya kuleta watu wanaokuja kupoteza muda na kwa kuwa viwango vyao si sahihi, wanaishia kuchota fedha ambazo wangefaidika nazo wazalendo na pia kuzalisha majungu tu.

Hatutaki majungu ya kigeni, tuliyonayo ya kizalendo yametuzidi uzito. Badala yake tunataka wageni washindani na waleta changamoto kwa wazawa ili tuweze kufikia malengo ya mabadiliko.

Kama wageni watashindwa kuonyesha changamoto au kuwa mifano ya kuigwa, basi ni bora kupunguza idadi ya wanaosajiliwa kama wageni ili tuweze kupata watu sahihi.
Katika hili, viongozi wa klabu za soka na makocha wakiwemo wa kigeni mnahusika katika sehemu fulani ambazo mnafanya ujanjaujanja.

Wachezaji wengi wanaoletwa kwenye klabu nyingi hasa kubwa za Yanga, Simba na Azam FC wanaonekana ni wa kuungaunga. Baadhi yao wameanza kupata kasi wakiwa ndani ya klabu hizo wakikaa benchi muda mwingi huku wazawa wakiendelea kucheza wakiwa wanalipwa kidogo, hili nalo si sawa.

Vizuri mnaohusika na usajili, angalieni suala la uzalendo kuanzia katika klabu zenu na pia taifa letu. Achaneni na mambo ya ‘ten percent’ ili tuweze kujenga nchi yetu katika upande wa soka. Kwani nyie ni watu wa aina gani hamchoshwi na maumivu ya klabu zetu na taifa letu kuendelea kuboronga?

Angalia yule kiungo wa Yanga Mniger anayeitwa Yossouf Boubacary ninaamini hana tofauti na mimi kiuchezaji kama nitaamua kucheza kwa kufanya mazoezi mwezi mzima nikiwa nimeweka malengo nataka kucheza ligi kuu kwa umri huu wa ‘kizee’. 

Simba nao walikuwa naye mtu kama Emiry Nimubona ambao hata wangeamua kwenda Abajalo ya Sinza wangempata mchezaji wa aina yake. Iko haja mlitafakari hili na tafadhari, acheni longolongo, mashabiki nao wanaumia pia, soka letu linaumia sana na sisi wadau tumechoka kuona wageni wasio na uwezo kulipwa na kufaidika kwa kiwango cha walio na uwezo.

1 COMMENTS:

  1. Sio kweli kwamba huyu jamaa Boubacary ni wa kiwango kidogo hata wewe unaweza kumzidi, ila ni lazima tukubali kuwa kwenye mfumo wa mwal hana nafasi kwa sababu hakabi ndo maana mwl anaprefer Kaseke!! Yule jamaa yuko vizuri na unaweza kuona kuwa ndo alitengeneza goli dhidi ya Al Ahly!! Tusilete dharau tu kwakuwa hana nafac kikosini, hata kwa Bossou mlisema sana lakini shughuri yake mnaiona!! Akina Shevshenko, Dimaria, Tores nk sio kwamba hawakuwa na viwango bali mfumo wa mwal ndo haukuwakubali ndo maana walikotoka walikuwa wanafanya vizuri. Mnapochambua tumieni weledi badala ya mihemuko na ushabiki!!

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV