Na Saleh Ally
MJADALA unaoendelea kushika kasi katika soka nchini ni mafanikio ya wachezaji kutoka Zimbabwe, namna wanavyoweza kuonekana lulu kwa kupata mafanikio katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Angalia Donald Ngoma na Thabani Kamusoko walivyofanya kazi nzuri kabisa na kuiwezesha Yanga kubeba ubingwa wa Bara pamoja na Kombe la FA lakini kufanikiwa kucheza robo fainali ya Kombe la Shirikisho.
Simba imeshika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Bara, lakini kati ya wachezaji wa kulipwa ambao wameonyesha walikuwa wana faida ni Justice Majabvi raia wa Zimbabwe pia.
Gumzo kubwa ni kwa nini wachezaji hao wanaofanya vizuri hapa nyumbani kwao wanaonekana kama hawana lolote kwa kuwa hawako katika timu yao ya taifa!
Kwa upande wa Ngoma, huenda washambuliaji wanaocheza soka nchini Afrika Kusini kama Khama Billiat na Cuthbert Mulajila ndiyo wanaonekana kupewa kipaumbele na kweli wameifanya kazi yao vizuri.
Lakini kama unazungumzia kiungo cha ukabaji ambayo ni namba ya Kamusoko na Majabvi, basi hakuna ambaye anaweza kucheza dhidi ya Willard Katsande, huyu ndiye nahodha wa timu ya taifa ya Zimbabwe.
Katsande ni shoka hasa, mchezaji ambaye sasa anakipiga katika kikosi cha Kaizer Chiefs cha Afrika Kusini na mmoja wa wachezaji wanaopewa thamani ya juu kama atatakiwa kuuzwa, thamani yake imefikia euro 550,000 (Sh bilioni 1.3).
Kwa muonekano, Katsande ni mtu ambaye ni nadra sana kutabasamu lakini unaweza kumuita “mkatili” na asiyetaka mchezo hata kidogo. Mjeuri wakati wa kukaba na ana akili wakati timu inaanza kusambaa kwenda mbele.
Ajax Cape Town walimuona baada ya kufanya kweli wakati akiichezea timu yake ya Gunners FC ya Zimbabwe ambayo iliitwanga Al Ahly kwa bao 1-0 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa mjini Harare, lakini ikapoteza kwa mabao 2-0 jijini Cairo na Al Ahly kufuzu kwa jumla ya 2-1.
Ajax alicheza msimu mmoja uliofuatia akatua Kaizer Chiefs aliyoanza kuichezea rasmi fainali ya Kombe la MTN 8 akiingia kuchukua nafasi ya Siphiwe Tshabalala. Hiyo ilikuwa ni Septemba 10, 2011.
Aliporejea katika ligi, katika mechi 12 za kwanza, Katsande alitandikwa kadi tano za njano na moja nyekundu! Hadi msimu unamalizika akashika chati ya kuwa mchezaji mwenye kadi nyingi zaidi za njano, pia moja nyekundu.
Kazi kwa benchi la ufundi la Kaizer Chiefs ikawa ni kupunguza makali kidogo ya uchezaji wake wa “kazikazi” na kumtengeneza katika mfumo wa mtu anayeweza kuchezesha kwa maana ya kusukuma timu.
Hiyo ilisaidia kidogo, lakini haikuweza kumfutia ule mfumo wake wa kucheza “shoka” kweli.
Ndani ya misimu mitatu, akiwa na Kaizer Chiefs, Katsande alifanikiwa kushinda tuzo za mwanasoka bora wa mwezi, mwanasoka bora wa msimu na mwanasoka bora wa mashabiki mtandaoni wa Kaizer Cheifs na kufanikiwa kubeba kitita cha randi 230,000 (zaidi ya Sh milioni 79).
Msimu huu, amekuwa nahodha mwenye mafanikio akiiwezesha Zimbabwe kufuzu kucheza Kombe la Mataifa Afrika chini ya Kocha Kalisto Pasuwa ambaye alionekana kuivutia Simba.
Katsande ambaye tayari amecheza dakika 2,363 katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini na dakika 390 katika michuano ya MTN 8 ni kisiki kweli, mtu asiyetaka mchezo akiwa kazini na ambaye anaifanya kazi yake kwa weledi kwa kuwa hataki kushindwa na dakika 90 za uwanjani, kwake ni kazi isiyotaka utani hata kidogo.
Kwa Wazimbabwe, Afrika Kusini kwao ni sawa na yule anayecheza Ulaya na idadi kubwa ya wachezaji wanaoaminika katika kikosi cha timu ya taifa ni wale wanaotokea nchini humo hasa katika timu nne kubwa za Orlando Pirates, Kaizer Chiefs, Ajax na Mamelodi Sundowns.
Katsande ndiyo anatoka hivyo, maana ana umri wa miaka 30 sasa. Lakini hakutakuwa na nafasi kwa Kamusoko au Majabvi kwa kuwa nao umri unawatupa mkono na kwa mwonekano, nahodha wao huyo ana nafasi ya kucheza misimu mingine mitatu au minne kwa ushindani wa juu namna hiyo.
Hivyo, unapouliza kwa nini Kamusoko ambaye ni injini ya Yanga na Majabvi ambaye anakipanga kikosi cha Simba kwenda mbele hawachezi, basi kumbuka jina la Katsande ambaye Wazimbabwe wanamwita, Farasi.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment