June 10, 2016


Na Saleh Ally
KATI ya viungo waliotikisa katika soka nchini ni Athumani Iddi, maarufu kama Chuji na mwendo uliopo, inaonekana sasa viungo wa aina yake kupatikana, imekuwa ni nadra.

Chuji aling’ara akiwa Simba, aling’ara akiwa Yanga, pia ni kati ya viungo waliofanya kazi ya ziada kupambana hadi Taifa Stars ikafanikiwa kucheza katika Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) mwaka 2009 nchini Ivory Coast.

Baadaye kiungo huyo alizimika kabisa, kukawa na tuhuma za ulevi na baadaye akapotea kabisa hadi alipoibuka na kujiunga na Mwadui FC ya Shinyanga ambayo aliichezea na kuisaidia kurejea Ligi Kuu Bara.

Baada ya timu hiyo kurejea Ligi Kuu Bara baada ya zaidi ya miaka 20, Chuji alishindwa kabisa kung’ara na kumekuwa na tuhuma nyingi likiwemo suala la utumiaji wa vilevi kupita kiasi.


Baada ya kufeli na kupotea kwa Chuji, inaonekana hakuna namba sita ambaye amekuwa na uwezo wa juu kama ilivyokuwa kwake kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

Je, Chuji bado ana hamu ya kucheza soka na kufanya vema, kweli vilevi vimemmaliza? SALEHJEMBE ilimtafuta na kugundua ni mtu ambaye amekuwa akifanya mazoezi sasa. Sasa vipi, mbona ameboronga akiwa na Mwadui, hata nafasi ya kucheza alikuwa hana!


SALEHJEMBE: Ninaamini umewahi kuwa mmoja wa viungo bora kabisa, vipi hata Mwadui umeshindwa kabisa kucheza, huu ndiyo mwisho wako?
Chuji: Nani kasema nimeshindwa kucheza? Kumbuka mimi siyo nimewahi, hata sasa ni kiungo bora kabisa.

SALEHJEMBE:Hauwezi kuwa kiungo bora ukiwa benchi. Hata Mwadui FC, umeshindwa kucheza?
Chuji: Kwa muonekano wa nje, lakini ukweli mambo kwangu hayakuwa mazuri hasa upande wangu. Lakini sipendi kuzungumza mambo na kuanzisha malumbano, hiyo si kazi yangu.

SALEHJEMBE: Unaonekana unafanya mazoezi mfululizo hata kipindi hiki cha mwezi mtukufu, unajiandaa na nini?
Chuji: Kwanza nataka kujiweka vizuri, kweli ninataka kucheza ligi kuu na kuonyesha uwezo wangu.

SALEHJEMBE: Kucheza si lazima upate timu, Mwadui umeshindwa unafikiri utaweza kuinuka tena?
Chuji: Siwezi kushindwa, masuala ya Mwadui tuyaache. Ninaamini kabisa nitapata timu na kuna baadhi ya timu zimeanza kuonyesha nia. Nataka nirejee na kuonyesha mfano wa namba sita inachezwa vipi.


SALEHJEMBE: Umri unakutupa mkono Chuji, vijana sasa wako tofauti. Utaweza kupambana nao?
Chuji: Misimu miwili iliyopita, nilikuwa kiongozi wa kuipandisha Mwadui FC. Hao vijana wamebadilika nini, wakati mwingine hata kwenda uwanjani siendi kwa kuwa sioni hao viungo wanafanya nini uwanjani. Pasi utafikiri wanafanya shoo, hazina malengo. Mara nyingi naenda uwanjani hadi nikisikia Haruna (Niyonzima) anacheza.

SALEHJEMBE: Unataka kusema ndiye pekee anapiga pasi za malengo kwa wachezaji wote wa ligi kuu?
Chuji: Huo ni mtazamo wangu, Haruna anaweza kubaki na mpira lakini akipiga pasi ujue kazi ipo. Haruna ana akili sana kwa mtu anayejua mpira.

SALEHJEMBE: Hukujibu swali langu kuhusu umri kukutupa mkono.
Chuji: Hili linaulizwa sana, watu wananilazimisha kuwa mzee. Sasa nina miaka 31, vipi nishindwe kucheza? Angalia Uganda, kina Massa, Mwesigwa na hata Kenya bado wapo wanaocheza na wana umri hadi miaka 36.


SALEHJEMBE: Kumbuka wao wana nidhamu, wewe uliwahi hadi kuingia kwenye kashfa ya utumiaji wa madawa ya kulevya!
Chuji: Tuhuma si lazima ziwe ukweli. Wakati mwingine unalazimika kunyamaza tu.

SALEHJEMBE: Unatumia kilevi gani kwa kipindi hiki?
Chuji: Najua nikisema utakataa, mimi sinywi hata pombe kwa sasa, sivuti sigara wala chochote. Huu ni mwezi mtukufu (anaapa). Nakwambia niamini, situmii kilevi chochote na nitaonyesha, wewe hifadhi maneno yangu.

SALEHJEMBE: Una maoni gani kuhusiana na Taifa Stars?
Chuji: Kwa mwendo huu hatutafika mbali. Kwanza watu hawapendani, pili hawaheshimiani. Hakuna watu wanaofanikiwa bila ya kuwa na vitu hivyo.


SALEHJEMBE: Unaweza kwenda kwa mifano?
Chuji: Angalia ishu ya Cannavaro, hadi amesusa. Ukweli ni kwamba walimdharau na wanakataa kukubali. Lakini yule ni muhimu sana, ana uzoefu na anaweza kuwa kiongozi. Wakati mwingine umri ni muhimu. Lazima uchanganye vijana na wakongwe, hamuwezi kuwa na timu ya taifa ya vijana tu, ni kujidanganya.

SALEHJEMBE: Kwani Samatta hauamini anaiweza hiyo kazi?
Chuji: Ndiyo anaiweza, lakini kuwa na Cannavaro ndani yake ingekuwa msaada kwake. Pia wachezaji wa nyumbani wajitume na kujitambua maana hata huyo Samatta naye wanamchosha tu, mwisho mtaona kama hawezi.

SALEHJEMBE: Ulizungumzia heshima, unaweza kufafanua kwa uwazi?
Chuji: Ndiyo, watoto wanavimba vichwa mapema. Alikuwa anapata laki tatu kwa mwezi, akiingia Yanga au Simba akalipwa laki nane au milioni, anaanza kujiona kama anacheza England. Mwisho inakuwa hakuna anayemheshimu mwenzake.

SALEHJEMBE: Labda katika heshima, wakati unachipukia ulikuwa unafanyaje?
Chuji: Niliingia timu ya taifa mwaka 2004. Hapo unawakuta watu kama akina Matola. Namba ngumu kweli, kila siku unakwenda mwenyewe kujifua beach. Lakini unawaonyesha heshima na kujifunza kwao, wao pia wanakuwa tayari kukusaidia. Lakini sasa kijana akiingia anataka wakongwe wamtazame yeye.


SALEHJEMBE: Nini faida ya wakongwe katika timu?
Chuji: Wana uzoefu, wanajua nini kifanyike na wakati gani. Nakumbuka tulikuwa tunacheza na Senegal kwao. Tuliwashambulia mfululizo kwa dakika 12 hivi. Nahodha wao akanyoosha mkono na kumpa ishara yule kipa Silva, ghafla akavua gloves zake na kulala chini kama kaumia.
Mpira ulisimama kwa dakika mbili, wakati anatibiwa wao walikuwa wanazungumza wameweka raundi.
Waliporejea, tulikuwa hatujui wa kumkaba. Maana ilikuwa ni hatari.1 COMMENTS:

  1. Binafs namkubali sana sana sana chuji,ana uwezo wa kucheza 6 lkn akamfunika 8 na tim ikaenda kwa pas zake ndefu zenye kufika.

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV