June 25, 2016

JUMA ABDUL
Yanga huenda ikashusha pumzi kidogo katika nafasi ya beki ya kulia kwani Juma Abdul ameanza mazoezi ya nguvu na jana Ijumaa asubuhi alicheza dakika 90 uwanjani.

Abdul aliumia kifundo cha mguu katika mchezo wa fainali ya Kombe la FA dhidi ya Azam FC hivi karibuni ambapo Yanga ilishinda mabao 3-1, siku alipoumia nafasi yake ilichukuliwa na Mbuyu Twite.

Alitibiwa na kupata nafuu lakini akajitonesha katika mchezo wa Taifa Stars na Misri wa kufuzu Kombe la Afrika 2017 na tangu hapo hakuonekana uwanjani, ambapo alikuwa akiuguza jeraha hilo.

Baada ya kufanya mazoezi ya ufukweni kwa wiki nzima, jana Abdul alifanya mazoezi ya uwanjani kwenye Uwanja wa Garden uliopo Vijana, Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo alitumia dakika 90.

SALEHJEMBE ilimshuhudia Abdul akianza na zoezi la kukimbia akizunguka uwanja mara 20 kabla ya kucheza uwanjani.

Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Abdul alisema: “Nipo fiti kabisa na ninaweza kucheza mechi na TP Mazembe, wiki nzima nilikuwa na programu ya mazoezi ya stamina katika Ufukwe wa Coco.

“Leo (jana) ndiyo nimeanza kucheza uwanjani na nimetoka freshi kabisa na sina shaka hata nikipewa mechi ya Mazembe.”

Wakati wenzake wakiwa kambini Antalya, Uturuki, beki huyo alikuwa chini ya uangalizi wa Daktari Haroun Ally.

Yanga itacheza na TP Mazembe, Jumanne ijayo mchezo wa Kundi A wa Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV