June 10, 2016


Beki mpya wa kulia wa Yanga, Hassan Kessy aliyejiunga na timu hiyo hivi karibuni akitokea Simba, amemwagia sifa kocha mkuu wa timu hiyo, Mholanzi, Hans van Der Pluijm.

Kessy ambaye jana Alhamisi ilikuwa ni siku yake ya tatu ya kujifua na kikosi cha Yanga tangu alipomwaga wino wa kuitumikia klabu hiyo, lakini ikiwa ni mara ya pili kufundishwa na Pluijm, alisema kuwa kwa jinsi alivyomuona kocha huyo mazoezini anaamini kiwango chake kitaongezeka zaidi ya alivyokuwa Simba.

Kessy alisema kuwa katika siku hizo mbili za kuwa chini ya Pluijm mazoezini amebaini  tofauti kubwa na makocha wengine waliyowahi kumfundisha akiwa Simba na Mtibwa Sugar.

 “Katika mazoezi yangu ya siku mbili nikiwa chini ya Pluijm, nimegundua kuwa ni kocha mzuri anayejua majukumu yake na ndiyo maana Yanga ilikuwa inafanya vizuri kwenye mechi zake za Ligi Kuu Bara na zile za Kombe la Shirikisho Afrika.

“Nimegundua kuwa hataki mchezo anapokuwa kazini na anataka kila mchezaji azingatie kile anachotaka akifanye bila ya kufanya utani, lakini pia ni mkali sana kwa mchezaji mvivu.

“Kwa hali hiyo, ni matumaini yangu kuwa Mungu akinijalia uzima basi msimu ujao nitakuwa vizuri zaidi ya nilivyokuwa Simba na Mtibwa Sugar,” alisema Kessy.

SOURCE: CHAMPIONI


1 COMMENTS:

  1. Hapo chacha!
    Umekubali kwamba Yanga sio ya kubebwa bali ni bidii na umakini kutoka kwa mwalimu?kaza buti dogo,vinginevyo utaishia kusugua benchi.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic