June 16, 2016


WAZIRI SIMBACHAWENE

Na Saleh Ally
Kati ya wadau ambao nimekuwa nikiwaona wakipambana kwa ajili ya michezo hasa mchezo wa riadha ni Gida Budayi.

Lakini leo amenishangaza alipokuwa akizungumzia msimamo wake kuhusiana na kusimamishwa kwa michezo ya Shule za Msingi na ile ya Sekondari maarufu kama Ummitashumta na Umiseta.

Siku tatu zilizopita, Waziri  wa Ofisi ya Rais ,Tamisemi, ,utumishi na Utawala bora,George Simbachawene alitangazwa kusitishwa kwa michezo hiyo kwa madai ya kutaka kutimiza agizo la Rais John Pombe Magufuli, kwamba hadi mwisho wa mwezi huu, kusiwe na mtoto anayekaa chini.

Gida Budayi alisema angependa kutofautiana na wadau waliolaumu kuhusiana na suala hilo. Akidai yeye anaona tofauti kwa kuwa kuna haja gani ya kulazimika kuwa na mbegu wakati huna shamba. Kwamba wale watoto wanaoshiriki michezo, wanapofanikiwa wanakwenda wapi wakati hakuna sehemu kama vile vituo vya michezo.

Mdau huyo katika mahojiano na Radio One alionekana kabisa alikuwa akilenga kuhusiana na mchezo wa raidha ambao yeye ni mdau mkubwa.

Msisitizo wake ni kwamba, hata kama watoto wakifanya vizuri, basi hakuna pa wa kuwapeleka. Mwisho akahoji hata soka vipi hawashiriki Olimpiki kama ilivyokuwa Nigeria iliyokuwa ya kwanza kushiriki enzi za kina Kanu.

Lakini Gida Budayi akaenda mbali zaidi  kwa kusema kuna maofisa elimu ambao wanakaa tu maofisini na ndiyo wamekuwa wakizitumia fedha hizo kujenga nyumba zao.

Nami niwe wazi, nionyeshe ninampinga mdau huyo kwa kusema hivi, nimekuwa nikiunga kwa nguvu zote mapambano yake ya kuinua mchezo wa riadha, lakini safari hii anaonekana alinuia kujipatia sifa au kutaka kusikika au kuona raha akiwa mtu mwenye upande usio na wengi bila ya kujali alizungumza mambo mengi sana ya kubahatisha, hakika sikutarajia.

Nianzie na alipoishia, lini amewahi kueleza uozo wa maofisa elimu kutumia fedha za michezo kama Umiseta au Ummitashumta kwa ajili ya kujenga nyumba zao?

Ajabu zaidi, anaanza kuzungumzia Olimpiki akiamini katika soka ndicho pekee kinachotafutwa! Hajui michezo hiyo imetoa wachezaji wangapi ambao leo wanaishi maisha mazuri maradufu!

Hajui kuna wachezaji waliopitia katika michezo hiyo, leo wanamiliki majumba na usafiri kwa kuwa walitafutwa. Hajui kulikuwa na shule kama Makongo ambayo ilijitolea kuwaendeleza na wengine wakawa shujaa wa taifa letu katika ngazi za klabu au taifa letu?

Najua Gida Budayi alipata elimu yake nje, huenda aliporejea hakujifunza mambo mengi sana aliyoyaacha nyuma na hakutaka kujua ndiyo maana hana uchungu na michezo hiyo ya shule za msingi na sekondari.

Wakati mwingine nilianza kufikiria Gida Budayi atakuwepo kwa ajili ya kupinga chochote atakachokitetea Filbert Bayi kwa kuwa tu amekuwa akitofautiana naye katika masuala ya riadha. 

Nimekuwa nikimuunga kwa pointi nyingi za msingi kuhusiana na riadha wakati akimueleza Bayi. Lakini katika hili, kama kweli kwa kuwa Bayi amepinga kusimamishwa kwa michezo hiyo, basi lazima yeye aibuke na kusema anaunga mkono, itakuwa ni kitu cha ajabu kabisa kuingia masikioni mwa wadau wa soka.

Angalia hapa, wakati yeye anasema anaunga mkono, mwisho anapishana na ilichokifanya serikali iliyoamua kununua madawati fedha za michezo hiyo. Yeye anasema anaunga mkono, huku akitaja kujengwa kwa vituo vya michezo. Sasa serikali kwani imejenga vituo vya michezo.

Lakini je, baada ya kusimamishwa mwaka huu, kama mwakani itakuwepo, vituo vya michezo vitakuwa vimekamilika? Naona ni maneno yasiyo na faida, sawa na mbegu zisizoweza kuzalisha mazao zilizopandwa shambani.

Vizuri wadau wa michezo tuangalie hili kwa jicho la tatu badala ya kila mmoja kutaka kujipatia sifa kwa kuzungumza tu ili mradi asikike. Kweli kila mmoja ana haki ya kutoa mawazo yake, lakini vizuri kutafakari kabla ya kuyatoa kwenye jamii.

Wamesema serikali imeokoa bilioni 1.5 kutoka kwenye Ummitashumta na Umiseta. Inaumiza sana kusikia kutofanyika kwa michezo ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ni kuokoa fedha!

Vipi mbona hawakusitiza Mwenge wa Uhuru, Vipi Hawakusitiza sherehe zote zinazohusiana na kuadhimisha ukiachana na il ya Uhuru. Kwani zile mwendelezo wake kwa maana ya maendeleo ni nini.

Serikali haina urafiki wala ukaribu na michezo, hata Sh bilioni 1.5 inayotoa kwa ajili ya wanafunzi hao nayo inaonekana inapotea? Kama inashindwa kufanya fainali tu za wanafunzi, itaweza vipi kutenga kiasi cha fedha kusaidia michezo nchini.

Michezo ni ajira, inaingiza kipato kwa taifa kupitia kodi. Lakini leo inaonekana eti kutofanyika kwake ni kuokoa fedha. 

Angalia katika soka, fedha zinaingia serikalini kupitia Kodi ya Mapato, inaingia kupitia viwanja, maana mapato yake yanakatwa na kadhalika. Vipi serikali inaona kutofanyika kwa michezo ni kuokoa fedha. Tena michezo ya wanafunzi ambao kila siku wanahimizwa kushiriki michezo.

Wangapi watakuwa wamekata tamaa na kuamua kuachana na michezo baada ya kuona serikali haithamini? Hakika huu ndiyo wakati wa kutafakari na wanaochangia wawe makini kuliko kutaka “kujionyesha” au kuzungumza kwa manufaa yao binafsi badala ya taifa letu.

Mimi naendelea kusisitiza, suala la vituo vya michezo ni zuri, suala la madawati ni zuri lakini hakukuwa na ulazima wa kuisimamisha michezo eti kuokoa fedha.


Kwangu naona ndani yake kuna uoga, waziri hakuwa mtulivu ili aweze kuhakikisha michezo hiyo inaendelea na madawati yanapatika. Hakutulia kufanya ubunifu au hakuwa tayari kufanya ubunifu na kilichofanyika sasa si sawa hata kidogo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic