June 17, 2016


Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala jijini Dar es Salaam, bado linaendelea kumsaka muuaji wa aliyekuwa beki wa kati wa Mtibwa Sugar, John Mabula pamoja na shemeji yake Ncheye Festo.

Mabula na Festo waliuawa kwa kuchomwa na kisu Jumamosi iliyopita huko Kitunda Kibeberu jijini Dar es Salaam wakiwa baa walipokuwa wameenda kunywa bia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lukas Mkondya, amesema kuwa jeshi hilo bado linaendelea kumsaka mtuhumiwa wa tukio hilo ili aweze kufikishwa katika mkono wa sheria.

Katika hatua nyingine, Msemaji wa Familia ya Mabula, John Mkune, aliliambia gazeti hili kuwa beki huyo ambaye ameacha mjane na watoto wanne wa kike, amezikwa jana huko nyumbani kwao Bushushu mkoani Shinyanga.

“Mabula tumemzika leo saa 10 jioni (jana) huku nyumbani kwao mkoani Shinyanga katika Kijiji cha Bushushu alikozaliwa.

“Hata hivyo, tunaliomba Jeshi la Polisi kuhakikisha linamtafuta muuaji ili aweze kufikishwa katika mkono wa sheria, kwani kitendo alichokifanya ni zaidi ya unyama,” alisema Mkune.

Juzi Jumatano, wapenzi na mashabiki wa soka hapa nchini wakiwemo wachezaji wenzake aliowahi kucheza nao soka alipokuwa Mtibwa Sugar, walijitokeza nyumbani kwake kitunda kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Mabula kabla ya kusafirishwa kwa gari kwenda kwao Bushushu, Shinyanga kwa ajili ya mazishi.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV