June 13, 2016


RAHIM JUMA

Huku uongozi wa Simba hivi sasa ukiwa katika harakati kabambe za kuhakikisha unakiimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara baada ya ule uliopita kufanya vibaya, huenda ukajikuta kwenye wakati mgumu baada ya timu ya Sofapaka ya nchini Kenya kuingilia harakati hizo za  uongozi huo.

Sofapaka inadaiwa kuingilia harakati za Simba baada ya timu hiyo nayo kuonyesha nia ya kutaka kumsajili beki wa kati wa African Sports ya Tanga, Rahim Juma ambeye pia anatakiwa na Wekundu hao wa Msimbazi.

Hivi karibuni iliripotiwa kuwa Simba inamtaka beki huyo ambaye msimu uliopita alionyesha kiwango kikubwa akiwa na kikosi cha African Sports ili kuiongezea nguvu safu yake ya ulinzi ambayo haikuwa sawa.

Akizungumza na Championi Jumatatu, mmoja wa viongozi wa African Sports ambaye aliomba kutotajwa jina lake, alisema kuwa Sofapaka tayari imeshabisha hodi klabuni hapo ikimtaka mchezaji huyo.

“Taarifa za Simba kumtaka Rahim tunazisikia tu labda kama wamezungumza naye yeye mwenyewe lakini tunachujua sisi ni kwamba Sofapaka ndiyo wanataka na walisema kuwa wanasubiria ligi yao isimame ili aweze kwenda kufanya majaribio.

“Hata hivyo, kama Simba wanamtaka basi wafanye kile kinachotakiwa ili waweze kumsajili kwa sababu tunachotaka sisi ni kuona kipaji chake hakipotei kwa sababu ni mchezaji mzuri,” alisema kiongozi huyo.


Alipotafutwa Rahim ili aweze kuzungumzia suala hilo hakuweza kupatikana lakini aliyekuwa kocha wake mkuu msimu uliopita, Ramadhan Aluko alisema: “Taarifa hizo za kwenda Kenya aliwahi kuniambia lakini kuhusu Simba bado hajaniambia.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV