June 13, 2016

DANTE (KULIA) AKIWA MAZOEZINI NA HAJI MWINYI.
Beki wa kimataifa wa Yanga, Mtogo, Vincent Bossou, bado hajajiunga na timu hiyo na kuibua hofu kubwa kwa mashabiki wa Yanga kuelekea katika mchezo wao dhidi ya MO Bejaia ya Algeria lakini bosi wa benchi la ufundi la Yanga, Hans Pluijm amewatuliza na kusema yupo Andrew Vincent ‘Dante’, hakuna kitakachoharibika.

Mpaka jana Alfajiri Yanga ilipoondoka kuelekea Uturuki kwa ajili ya kambi kabla ya mchezo wao huo wa kwanza wa makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, bado hakukuwa na taarifa rasmi za ujio wa beki huyo, ikiaminika kuwa anaweza kuungana na kikosi hicho nchini Algeria siku chache kabla ya mechi.   

Beki wa kati mwingine na nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ hataweza kucheza mechi hiyo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata walipokuwa wakiumana na Sagrada Esparanca ya Angola.

Pluijm amesema kuwa hana taarifa kamili kuhusiana na Bossou lakini hilo halimpi shida kwa kuwa wapo wanaoweza kuchukua nafasi yake na mambo yakaenda sawa akiwemo beki wa kazi, Dante aliyesajiliwa hivi karibuni kutoka Mtibwa Sugar na mkongwe Mbuyu Twite.

“Sijui vizuri kuhusiana na Bossou lakini hilo siwezi kuliangalia zaidi kwa sasa kwa kuwa nina wachezaji wengine ninaotakiwa kujipanga nao kwa ajili ya mechi ijayo, uzuri ni kwamba hapa kuna watu watakaoziba hiyo nafasi bila tatizo.

“Yupo Dante na wengine wanaweza kucheza na tukawa vizuri kutegemeana na mfumo na jinsi tutakavyohitaji kucheza tukiwa Algeria,” alisema Pluijm raia wa Uholanzi mwenye kadi ya uanachama wa Klabu ya Yanga.


Hata hivyo, taarifa nyingine kutoka kwa Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, inaeleza: “Bossou bado hajaja na sidhani kama tutakuwa naye Uturuki, nafikiri anaweza kujiunga nasi Algeria.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV