June 1, 2016

Uongozi wa Yanga umetamka kuwa utamsajili mshambuliaji wa kutegemewa wa Azam FC Muivory Coast, Kipre Tchetche pale ripoti ya kocha mkuu wa timu hiyo Mholanzi, Hans van Pluijm itakapoonyesha kuwa anamhitaji kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Hiyo ni siku chache tangu kuwepo kwa tetesi za mshambuliaji huyo kusaini kuichezea Yanga huku akiwa ameshamaliza mkataba na Azam.

Yanga tayari imefanikiwa kumsajili beki wa pembeni wa Simba, Hassani Kessy, aliyekuwa anakipiga Simba na Juma Mahadhi wa Coastal Union waliosaini mkataba wa miaka miwili kila mmoja.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, alisema sekretarieti ya Yanga bado haijapokea ripoti kutoka kwenye benchi la ufundi, hivyo ni ngumu kuzungumzia usajili kwa ujumla.

Muro alisema baada ya kupokea ripoti hiyo ya mapendekezo ya usajili atakayoyatoa kwenye ripoti yake katika kamati ya utendaji, ndiyo watajua kipi cha kufanya kuhakikisha wanafanya usajili bora utakaoipa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Aliongeza kuwa, katika ripoti hiyo watakayoipokea kutoka kwenye benchi hilo kama likiwepo jina la Tchetche, basi kamati ya utendaji itafanyia kazi kwa kuhakikisha wanaipata saini ya mshambuliaji huyo.

“Tchetche ni mchezaji mzuri ambaye ni aina ya wachezaji ambao tunahitaji kuwa nao Yanga kutokana na uwezo wake mkubwa alionao wa kufunga mabao.

“Kiukweli hadi sasa hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika kati yetu Yanga na mchezaji huyo, niongee ukweli, lakini kama kwenye ripoti ya benchi la ufundi ikionyesha kumhitaji, basi tutavunja benki na kumsajili.


“Hakuna kitakachotushinda kumsajili Tchetche, tunao viongozi bora kabisa watakaoweza kufanikisha usajili wa mshambuliaji huyo, ninaamini kama tukimpata atatusaidia kutokana uwezo wake,” alisema Muro.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV