June 1, 2016


Ishu ya Simba kupata kocha mpya imeingia kwenye sura mpya baada ya kulazimika kuandaa safari ya kwenda nchini Zimbabwe kumalizana na kocha waliyenaye kwenye mazungumzo, Mzimbabwe, Kalisto Pasuwa.

Hiyo imekuja baada ya kubainika ugumu wa vipengele vya mkataba aliokuwa nao kocha huyo wa timu ya taifa ya Zimbabwe.

Taarifa za ndani kutoka kwenye sekretarieti ya Wekundu hao, zimeeleza kuwa mazungumzo ya moja kwa moja na Pasuwa yamekwenda vizuri na yeye hana tatizo la kuja kuinoa Simba, kilichobaki ni mazungumzo ya Simba na wadhamini wa timu ya Zimbabwe wanaotajwa kumlipa stahiki zote Pasuwa akiwa na timu ya Zimbabwe.

Imeelezwa zaidi kuwa kiongozi mmoja kutoka kwenye kamati ya ufundi ndiye atakayepewa jukumu hilo la kwenda Zimbabwe wiki ijayo kuzungumza na wadhamini hao kupitia wakala wa kocha huyo kwa ajili ya kumaliza dili hilo.

“Yaani hapa ishu ya mazungumzo na huyu kocha imekwenda vizuri lakini sasa yeye ana mkataba na wadhamini wa timu ya taifa, hivyo kilichopangwa ni kutumwa mtu akazungumze na wakala wa huyu kocha kwa ajili ya kulimaliza hili na tumalizane na kocha pia,” kilisema chanzo hicho.

Katika hilo, ikalazimika kutafutwa, Bosi wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe ambapo alisema kwa sasa hawezi kuzungumza chochote.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV