June 6, 2016Rasmi kesho Jumanne, beki mpya wa timu ya Yanga, Hassan Kessy ataanza kufanya mazoezi na timu hiyo kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa kwanza wa makundi wa Kombe la Shrikisho Afrika.

Yanga itaanza kampeni zake za makundi kwa kuvaana na Mo Bejaia ya Algeria mchezo unaotarajiwa kupigwa Juni 17, mwaka huu.

Kessy ambaye ametua Yanga hivi karibuni na kupewa mkataba wa miaka miwili akitokea Simba, ataungana na wachezaji wengine wa klabu hiyo inayonolewa na Mholanzi, Hans van Pluijm, baada ya kupewa mapumziko ya takribani wiki moja na nusu.

Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, amesema kambi hiyo itaanza rasmi Jumanne huku wachezaji wote waliopo nchini na nje ya nchi wakitarajia kuanza kuingia leo Jumatatu kabla ya kuanza kwa maandalizi yao hayo.

“Rasmi tunaanza kambi yetu Jumanne (kesho), kwa ajili ya kuanza kujiandaa na michezo ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, kambi hiyo itaanzia hapahapa Dar na wachezaji wataanza kuwasili kesho (leo) Jumatatu kwa wale wa ndani na nje ya nchi.

“Wachezaji wetu wote wapya ikiwemo Hassan Kessy naye pia anatarajia kuwa miongoni mwa hao kwa sababu ni mchezaji wetu na tumemsajili tayari, hivyo ni lazima awepo katika kambi yetu hiyo,” alisema Hafidh.


Yanga imepangwa Kundi A, pamoja na timu za MO Bejaia ya Algeria, Medeama (Ghana) na TP Mazembe (DR Congo).

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV