July 18, 2016


Straika wa Yanga, Mzambia, Obrey Chirwa, ametamka kuwa mashabiki wa timu hiyo wanatakiwa kumpa muda kwa ajili ya kuendelea kuzoea mazingira ndani ya kikosi hicho kabla ya kuonyesha makali yake ambayo yalilifanya benchi la ufundi la timu hiyo kumsajili.

Chirwa mpaka sasa amefanikiwa kushuka dimbani kuichezea timu hiyo mara mbili katika michezo baina ya TP Mazembe na Medeama ya Ghana lakini katika michezo yote hiyo ameshindwa kufunga bao lolote.

Katika mchezo wa juzi dhidi ya Medeama, Chirwa alikosa nafasi nyingi za wazi na kupata lawama nyingi kutoka kwa mashabiki wa Yanga kwenye mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 na kuiweka Yanga katika mazingira magumu zaidi ya kusonga mbele.

Chirwa ambaye ametokea Klabu ya FC Platinum ya Zimbabwe, aliyotokea mshambuliaji mwingine wa timu hiyo, Donald Ngoma na kiungo Thaban Kamusoko, amesema kuwa, licha ya mashabiki wa timu hiyo kuendelea kumlaumu kutokana na kushindwa kuibeba timu hiyo, kwa upande wake anaomba wampe muda kabla ya kuonyesha thamani yake.

“Siyo kama nashindwa kufanya vyema, bado naendelea kujifunza mambo mengi ndani ya timu na hata kama unavyoona nakuwa napambana kwa uwezo wangu wote kuisaidia timu lakini mambo tu ndiyo yanakuwa tofauti, lakini kikubwa ambacho nawaomba mashabiki wa Yanga, ni kwamba waendelee kuwa wavumilivu kabla ya mambo kuwa mazuri hapo baadaye.


“Sijaona tatizo lolote kwetu licha ya mpaka sasa kutofanikiwa kushinda mchezo wowote ule katika Kombe la Shirikisho. Naamini bado tuna nafasi ya kufanya vyema kama tukijipanga katika michezo ijayo kwani hatujakata tamaa na imani yetu ni kwamba tuna nafasi ya kutinga nusu fainali,” alisema Chirwa. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV