July 18, 2016


Na Saleh Ally
TAYARI mabingwa wa soka Tanzania, Yanga wameshacheza mechi tatu za Kundi A katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na wamefanikiwa kupata pointi moja inayowafanya wakae mkiani.

Kundi hilo lina Timu za TP Mazembe ya DR Congo, MO Bejaia kutoka Algeria na Medeama kutoka Ghana ambayo iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi mbili baada ya kupata sare mbili.

Yanga ambayo ni timu pekee kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki kufikia katika hatua hiyo msimu huu, iko mkiani ikiwa na pointi moja. 

Awali baada ya ratiba ya makundi kutangazwa, asilimia kubwa ya uchambuzi au makisio yalikuwa hivi; TP Mazembe ilikuwa na uhakika wa kufuzu, hakuna aliyekataa na wengi waliamini Yanga ingeweza kupambana na MO Bejaia na Medeama na kufuzu kwenda nusu fainali.

Mechi tatu ilizocheza Yanga tayari ni kipimo tosha kwa kuwa sasa mambo ya kubashiri hayapo tena. Kila mmoja ameziona TP Mazembe, MO Bejaia na Medeama, ni timu za namna gani na inakuwa rahisi sana sasa kupima kwa kuwa hakuna haja ya kupima urefu wa kina cha mto kwa kutupia kijiti.


Katika mechi tatu ambazo Yanga imecheza, imefungwa mbili na kutoka sare moja. Katika mechi hizo imefungwa mabao matatu na kufunga moja tu. Kitakwimu utaona imefeli sehemu kubwa kabisa.
Katika mabao mawili iliyofungwa, imefungiwa nyumbani. Ugenini imefungwa moja na haijafunga hata bao moja ugenini. Nyumbani imeambulia sare na kufungwa.

Lakini ukizungumzia uchezaji, utaona Yanga ilikuwa katika kiwango bora kabisa kwa maana ya kumiliki mpira, kutengeneza nafasi na ikapoteza mambo mawili muhimu sana ambayo katika ‘level’ waliyonayo yanakuwa muhimu kuliko inavyokuwa kwenye ligi ya nyumbani.

Yanga imekuwa dhaifu kwenye ulinzi. Tena inaonekana ina makosa mengi sana inapokuwa inashambuliwa kwa mipira ya adhabu au ile ‘iliyopoa’ kwa kuwa mabao mawili iliyofungwa yametokana na mipira hiyo.

Faulo dhidi ya TP Mazembe ilizaa bao, ingawa bado lina utata hadi sasa, lakini utaona bao la Medeama lililoanzia na kona, linakwenda kuimaliza Yanga kwa ulaini kabisa!
Pili ni umakini ambao unaendana na vitu viwili, moja upande wa walinzi na pili upande wa washambuliaji. Ukianza na walinzi ni kushindwa kuwa na umakini wa mwendelezo.

Wakati wa mipira ya faulo, Yanga walishindwa kuwa makini katika mechi dhidi ya TP Mazembe. Hata kama kulikuwa na utata wa ‘offside’ bado hata wao hawakuwa wamekaba ‘ng’adu kwa ng’adu’ na kuwanyima pumzi TP Mazembe washindwe kabisa kufunga. Hilo ndilo lililotokea katika mechi ya juzi dhidi ya Medeama.


Yanga, wameshindwa kuwa makini kwa kuwa inaonyesha wakati mfungaji anafunga, alikuwa kazungukwa na mabeki watano wa Yanga lakini bado aliweza kufunga kwa kuwa kati ya mabeki hao wote, hakuna aliyekuwa anamkaba. 

Hata Vincent Bossou aliyekuwa karibu na Bernard Danso Ofori aliyefunga, hakuwa mwepesi kuufikia mpira kabla ya mshambuliaji huyo. Katika boksi, formula inasema; “Beki ndiye wa kwanza kuupiga au kuugusa mpira.”

Upande wa pili wa umakini ni ushambulizi, Yanga walipoteza nafasi zaidi ya mbili dhidi ya Bejaia wakiwa ugenini. Wakafanya hivyo dhidi ya TP Mazembe kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Wamerudia juzi, nikukumbushe tu nafasi hizi tatu ni za Amissi Tambwe, Obey Chirwa na Donald Ngoma.

Nafasi ya Yanga sasa unaweza kusema ni asilimia 10 ikitegemea miujiza ya soka. Lakini ukitanguliza ukweli, jibu litakuwa Yanga haina nafasi kwa kuwa inaonekana haijaiva kwa ajili ya michuano hiyo.

Haijaiva kwa kuwa makosa yanayofanyika yanaonekana kuwa ni ya ‘level’ ya Ligi Kuu Bara au yanaweza kuwa ni yale ya kiwango cha Kombe la Kagame ambalo linafanyika Afrika Mashariki na Kati.


Yanga imeingia anga nyingine ambazo inatakiwa kujifunza na kuthibitisha ule usemi wa kosa moja, bao moja. Unapokutana na watu walio makini au wanaojua mpira, hakika hawawezi kufanya utani.

Unaweza kusema Yanga ina wachezaji wa nje ya Tanzania. Kweli ni wazuri, lakini unarudi palepale, wanatokea Zimbabwe na Burundi ambao kweli hawana tofauti kubwa na Tanzania kwa kuwa wanatokea katika ukanda uleule. Tunajua Ukanda wa Kaskazini na Magharibi mwa Afrika ndiko soka lipo juu.


Lakini hata Bossou anayetokea Togo, bado nchi yake imeporomoka, naye si beki wa kiwango cha juu cha kutisha. Uzuri wake ni wa kupanda na kushuka, mechi hii juu, ile chini. Lakini makosa yake mengi ambayo amekuwa akiyafanya yanakuwa ni adhabu kubwa, kama hilo la kushindwa kuuwahi mpira ndani ya 18 akiwa amekaa na fowadi bila ya kumkaba, naye akamalizia kwa ulaini na kupata bao ‘laini ile mbaya’.

Yanga imepiga hatua kubwa, hili wote tunapaswa kulitambua na kulikubali. Tunajua timu za Tanzania kufikia hapo ni zaidi ya miaka nane iliyopita na Yanga ilijitahidi kufika lakini ikateleza kwa misimu miwili mfululizo.

Sasa kama kuna aliyefikiri ikifika basi lazima ivuke tena hadi nne bora, alikosea. Lazima kulitakiwa umakini na upungufu wa makosa, jambo ambalo zaidi huletwa na jambo moja kuu, ubora ambao pia hujengwa na ushiriki sahihi.

Huenda Yanga ingeweza kufanya vizuri zaidi kama itaingia hatua nyingine. Lakini safari hii, inaonekana ‘Mzigo mzito wa Mnyamwezi waliopewa, umekuwa mzito, umewazidi’. Kikubwa ni kuanza upya na uzoefu wa msimu huu, unaweza ukawa chachu ya kufanya vizuri katika michuano ijayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Takwimu zinaifunga Yanga, kwamba hatua hii ilikuwa ni ya juu kwake na inaweza ‘kujaribu tena’. Lakini viongozi, makocha na wachezaji wanaweza pia kuchagua, kujifunza au kukubali kufeli ili wasifeli tena itakapofikia wakati mwingine.

Katika soka, hakuna linaloshindikana. Lakini pia ukweli unakuwa una nguvu kuliko hisia za kudhani au kuona tu inawezekana na kulazimisha kuukimbia ukweli unaoonyesha kilicho wazi. 



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic