July 23, 2016



JOSEPH OMOG
Na Saleh Ally
KAZI rasmi ya Ligi Kuu Bara inaanza Agosti 20, mwaka huu na ndiyo kitakuwa kipimo cha karibu kila timu iliyo katika maandalizi wa msimu mzima.

Makocha watatu, walio Yanga, Simba na Azam FC, ndiyo wanakuwa na presha kubwa ya kuhakikisha timu hizo zinaendeleza utawala wao.

Timu zote tatu, zimewapa makocha wao mkataba wa miaka miwili. Hans van Der Pluijm, raia wa Uholanzi, yeye ameongezewa miaka miwili baada ya miaka miwili ya mafanikio Yanga.

Joseph Omog kutoka Cameroon, yeye ni mgeni Simba, amepewa mkataba wa miaka miwili kama ilivyo kwa Zeben Hernandez kutoka nchini Hispania.

Zeben anaweza kuwa na deni pia lakini Omog anaweza akawa na mengi ya kumpasua kichwa na utaona anaanza na ratiba yenye mfumo wa kupanda mlima, huenda mteremko akaukuta baadaye.

Tayari ratiba ya Ligi Kuu Bara imeshatoka, Simba itacheza mechi zake 15 za mzunguko wa kwanza kuanzia Agosti 20 hadi Novemba 6, mwaka huu kama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halitatupia viporo vyao kama ilivyozoeleka.

Ratiba hiyo inaonyesha wazi kuwa inamlazimisha Omog kuanza ligi kwa gia kubwa kwa kuwa kama atalegeza kamba kidogo tu, Simba inaweza kutumbukia kwenye dimbwi la sare mfululizo au kuambulia vipigo vya mapema ambavyo vitawapoteza kabisa.

Unaiona ratiba hiyo ina raha chache kwa Simba, lakini itakuwa na rundo la karaha kwa maana ya ugumu ambao kama kikosi cha Omog kitauweza, basi kitakuwa na nafasi ya kumaliza mzunguko huo vizuri zaidi.

Katika mechi 40 za mwanzo za msimu, yaani kuanzia Agosti 20 hadi Oktoba Mosi, Simba itakuwa imecheza mechi zote tatu kubwa ikianza na Mtibwa Sugar, Azam FC na Yanga.

Utaona ligi inaanza Agosti 20 lakini Simba inaanza mechi kubwa ya kwanza Septemba 9 dhidi ya Mtibwa Sugar, mechi inayofuata Septemba 17 wanawavaa Azam FC na siku tisa baadaye au kumi kasoro, Simba watakuwa wanakutana na Yanga.

Ndani ya siku hizo 40, pamoja na kucheza na Mtibwa, Azam FC na Yanga, Simba watakuwa wamecheza mechi saba za ligi na kubaki na nyingine nane.

Hii ni uthibitisho kwamba Omog atakuwa na presha kubwa ndani ya siku hizo 40 za mechi saba za ligi ambazo ndani yake anakutana na vigogo watatu.



Timu hizo tatu licha ya kuwa vigogo lakini ni zile zilizounda tano bora ya msimu uliopita, hii inamfanya Omog licha ya kutokuwa mgeni wa kombe la ligi hiyo lakini lazima awe na presha kubwa.

Kila kocha angependa kukutana na timu ambazo zingekuwa na ahueni kwa maana ya kujenga kikosi imara kabla ya kuanza kukutana na timu vigogo kidogo.

Wakati mechi hizo saba ni ndani ya siku 40, mechi tatu za Mtibwa, Azam na Yanga zenyewe zinakuwa ndani siku 20 tu, takriban wiki tatu ambayo ni presha kubwa sana kwa Simba.

Unajua unapotoka kukutana na timu ngumu kama Mtibwa, halafu unakwenda kukutana na Azam FC na baada ya hapo, siku saba tu unakutana na mtani ambaye ni presha kubwa kwa kuwa msimu uliopita alifanya vizuri ikiwa ni pamoja na kukufunga mara mbili, presha inakuwa juu zaidi.

Omog lazima aanze na gia kubwa ili kupanda kilima hicho kwa kasi. Kama atafeli ndani ya siku hizo 40, huenda msimu ukawa ni mgumu zaidi kwake kwa kuwa hali ya kutojiamini itashuka na kuifanya Simba kutomaliza vizuri mzunguko wa kwanza.

Kama Simba itafanikiwa kushinda mechi angalau tano katika saba halafu ikafanikiwa kuwafunga wakubwa wenzao kama Yanga, Mtibwa na Azam FC, basi itakuwa ni mwanzo mpya wa mabadiliko.

Kwani timu kama Simba inapokutana na wakubwa na kuwafunga maana yake itakuwa imejikusanyia pointi tatu kwa kila mmoja na kumkosesha pointi tatu. Kwa kuwa wao ndiyo wapinzani kileleni, itakuwa ni sawa na kupiga ndege wawili kwa jiwe moja.


Hata hivyo, haitakuwa kazi rahisi kwa Omog kwa kuwa Yanga wako vizuri ingawa si kweli kwamba hawatafungika. Lakini atakuwa na nafasi nzuri ya kukutana na makocha wengine wawili wageni ambao ni Hernandez akiwa na Azam FC pamoja na yule atakayekuwa Mtibwa Sugar, mfano ni Salum Mayanga.

Simba ina nafasi ya kufanya vizuri na itakuwa na nafasi ya kuchagua haya mawili. Kufanya vizuri irudishe heshima na Omog aone analiweza soka la hapa nchini, au iboronge ipotee kabisa kwa kuwa utakuwa ni msimu wa tano wa kucheza makidamakida.



RATIBA YA SIMBA MZUNGUKO WA KWANZA   
Agosti 20, 2016
Simba                  vs      Ndanda FC                   Taifa
         

Agosti 27, 2016
JKT Ruvu           vs      Simba                  Taifa



Septemba 7, 2016
Simba                  vs      Ruvu Shooting   Taifa

Septemba 11, 2016
Simba                  vs      Mtibwa Sugar     Taifa


Septemba 17, 2016
Azam FC             vs      Simba                  Taifa

Septemba 24, 2016
Simba                  vs      Majimaji Fc        Taifa


Oktoba 1, 2016
Yanga                  vs      Simba                  Taifa



Oktoba 8, 2016
Prisons                vs      Simba                  Sokoine (ITAPANGWA)

Oktoba 12, 2016                                                         
Mbeya City         vs      Simba                  Sokoine    

Oktoba 15, 2016
Simba                  vs      Kagera Sugar      Taifa

Oktoba 20, 2016
Simba                  vs      Mbao FC             Taifa

Oktoba 23, 2016
Simba                  vs      Toto African       Taifa

Oktoba 29, 2016
Mwadui fc          vs      Simba                  Mwadui Complex                

Novemba 2, 2016
Stand United      vs      Simba sc              kambarage
    
Novemba 6, 2016
African Lyon      vs      Simba                  Taifa



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic